51 - 75
51. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyo kwisha tangulizwa na
mikono yenu, na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.
52. Kama ada ya watu wa Firauni na walio kuwa kabla yao -
walizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa sababu
ya madhambi yao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na mkali wa kuadhibu.
53. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa
neema alizo waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao.
Na hakika Mwwnyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
54. Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao -
walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi yao.
Na tukawazamisha watu wa Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu.
55. Hakika vinyama vilio viovu kabisa mbele ya Mwenyezi
Mungu ni wale wanao kufuru, basi hao hawaamini;
56. Wale ambao miongoni mwao umepatana nao ahadi, kisha
wanavunja ahadi yao kila mara, wala hawamchi Mungu.
57. Basi ukiwakuta vitani wakimbize walio nyuma yao ili
wapate kukumbuka.
58. Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie
ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini.
59. Wala wasidhanie wale walio kufuru kwamba wao
wametangulia mbele. La, wao hawatashinda.
60. Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi
walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui
zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa
chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi
hamtadhulumiwa.
61. Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee
Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
62. Na wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu
atakutosheleza. Kwani Yeye ndiye aliye kuunga mkono kwa nusura yake na kwa
Waumini.
63. Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote
viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye
aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
64. Ewe
Nabii! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea wewe na Waumini walio kufuata.
65. Ewe
Nabii! Wahimize Waumini wende
vitani. Wakiwapo kati yenu ishirini wanao subiri watawashinda mia mbili. Na
wakiwapo kati yenu mia watawashinda elfu moja katika walio kufuru. Kwa sababu
wao ni watu wasio fahamu.
66. Sasa
Mwenyezi Mungu amekupunguzieni, na anajua kuwa upo udhaifu kwenu. Kwa hivyo
wakiwa wapo watu mia moja kati yenu wenye kusubiri watawashinda mia mbili. Na
wakiwapo elfu moja watawashinda elfu mbili, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
67. Haimfalii
Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika nchi. Mnataka
vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mtukufu
Mwenye nguvu Mwenye hikima.
68. Lau isingeli
kuwa hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu ingeli kupateni
adhabu kubwa kwa vile mlivyo chukua.
69. Basi kuleni
katika mlivyo teka, ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
70. Ewe
Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi akiona kheri yoyote
nyoyoni mwenu atakupeni bora kuliko vilivyo chukuliwa kwenu, na atakusameheni.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
71. Ikiwa
wanataka kukufanyia khiana, wao walikwisha mfanyia khiana Mwenyezi Mungu kabla
yake, na Yeye akakuwezesha kuwashinda. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye
hikima.
72. Hakika
wale walio amini na wakahama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao
na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki
na walinzi wao kwa wao. Na wale walio amini lakini hawakuhama, nyinyi hamna
waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu
katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo
mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
73. Na
wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipo fanya hivi itakuwako
fitna katika nchi na fisadi kubwa.
74. Na walio
amini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio toa
mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata msamaha wa
Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema.
75. Na
watakao amini baadaye na wakahajiri, na wakapigana Jihadi pamoja nanyi, basi
hao ni katika nyinyi. Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe
zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua
kila kitu.
|