9. SURATUT TAWBA
(Imeteremka
Madina)
Suratut
Tawba iliteremka Madina katika mwaka wa tisa wa Hijra, yaani miaka tisa baada
ya Mtume s.a.w. kuhamia Madina. Akaichukua Sura hii Ali bin Abi Talib r.a.
kuwapelekea Waislamu katika Hija na akawasomea. Na amir, yaani mwongozi, wa
Hija hiyo alikuwa Abu Bakr Assidiq r.a. Na Aya zake ni 129. Imeanzia kwa
kujitenga Mwenyezi Mungu Mtukufu na washirikina. Na kwa hivyo ikaitwa pia Sura
ya Baraa-ah, yaani kujitenga, kutokuwa na dhima, kutokuwa na jukumu. Na baada
ya hayo ikataja utakatifu wa miezi mitakatifu, na ahadi za washirikina, na
ipasavyo kutimiza ahadi nao ikiwa wao hawajaivunja. Na mwenye kuvunja ahadi
yapasa kupigana naye. Na baada ya hayo ikabainisha kuwa kiini cha kutaka
kumkaribia Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kumuamini Yeye. Na Imani haikamiliki ila
akiwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapendwa na Waumini kuliko kila kitu. Naye
Subhanahu ametaja kuwa kujiona una nguvu ndio kunapelekea kuwa mbali ushindi,
na akaashiria mfano wa vita vya Hunayni. Katika Sura hii wamepigiwa marfuku
washirikina wasiingie katika Msikiti Mtakatifu wa Makka, kwa kuwa wao ni
najisi!
Na katika Sura hii imetajwa kupasa kuwapiga vita Mayahudi na Wakristo mpaka
watoe jizya, kodi ya kichwa, na imebainishwa idadi ya miezi mitakatifu. Na humu
imebainishwa dharura ya kutoka kwenda vitani kila vikinadiwa bila ya
kulegalega. Na humo imeashiriwa hukumu ya wanao bakia nyuma, na walemevu wasio
weza kwenda kupigana, na imebainishwa hali ya wanaafiki ambao wanatafuta fitna
kila wakati vinapo nadiwa vita. Na Mwenyezi Mungu akataja wanaafiki wanavyo
watendea Waumini wakati wa salama na vita.
Katika Sura hii iko amri ya kukata iliyo tangazwa kuwatia adabu wanaafiki. Nayo
ni kuwa Mtume s.a.w. asimsalie yeyote katika wanaafiki akifa. Naye Subhanahu
ametaja udhuru unao mstahikia mtu kubaki nyuma asende vitani. Na pia Subhanahu
ameeleza hali ya wale mabedui walio dhihirisha kuingia katika Uislamu, au
wakafuata hukumu zake, baada ya kuwa Uislamu umepata nguvu. Na akaeleza kuwa
hao mabedui wako kando kando ya Madina.
Na baada ya hayo ametaja hali za watu kwa mnasaba wa Imani. Na akataja khabari
ya Msikiti wa Madhara walio ujenga wanaafiki ili upuuzwe Msikiti alio ujenga
Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. Kisha Subhanahu akataja sifa za Waumini walio
wakweli katika Imani yao, na toba ya wale walio mkhalifu Mtume wa Mwenyezi
Mungu s.a.w., na Mwenyezi Mungu akakubali toba hiyo, kama alivyo taja Subhanahu
wa Taa'la hali za watu katika kuzipokea Aya za Qur'ani zinapo teremka. Na
Subhanahu wa Taala akakhitimisha Sura hii kwa kusema kuwa hakika Mwenyezi Mungu
Mtukufu amemteua Muhammad kwa kumpa Utume, na kwamba yeye hawatakii shida hao
alio tumwa kwao, na kwamba yeye ni mpole na mwenye huruma kwao, na kwamba ikiwa
wakigeuka basi Mwenyezi Mungu anamtosheleza. (Angalia: Sura hii peke yake ndiyo
haianzii kwa Bismillahi, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu.)
|