1 - 50
1. Huku ni
kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwenye jukumu la maagano na mlio ahidiana
nao katika washirikina.
2. Basi
tembeeni katika nchi miezi mine, na jueni kwamba nyinyi hamwezi kumshinda
Mwenyezi Mung, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anaye wahizi makafiri.
3. Na ni
tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa
kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa washirikina. Basi mkitubu
itakuwa kheri kwenu, na mkigeuka basi jueni kuwa nyinyi hamumshindi Mwenyezi
Mungu. Na wabashirie makafiri kuwa watapata adhabu chungu.
4. Isipo
kuwa washirikina ambao mliahidiana nao kisha wasikupunguzieni chochote, wala
hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda wao.
Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wacha-Mungu.
5. Na
ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote mwakutapo, na washikeni
na wazungukeni, na wavizieni katika kila njia. Lakini wakitubu, wakashika Sala,
na wakatoa Zaka, basi waachilieni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
Mwenye kurehemu.
6. Na
ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate
kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani.
Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.
7. Itakuwaje iwepo ahadi na washirikina mbele ya Mwenyezi
Mungu na mbele ya Mtume wake, ila wale mlio ahidiana nao kwenye Msikiti
Mtakatifu? Basi maadamu wanakwenda nanyi sawa, nanyi pia nendeni sawa nao.
Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu
8. Itakuwaje! Nao wakikushindeni hawatazami kwenu udugu
wala ahadi. Wanakufurahisheni kwa midomo yao tu, na nyoyo zao zinakataa hayo.
Na wengi wao ni wapotovu.
9. Wamenunua thamani ndogo kwa Ishara za Mwenyezi Mungu, na
wakazuilia watu na Njia yake. Hakika hao ni maovu waliyo kuwa wakiyatenda.
10. Hawatazami kwa Muumini udugu wala ahadi; basi hao ndio
warukao mipaka.
11. Basi wakitubu na wakashika Sala na wakatoa Zaka, basi
ni ndugu zenu katika Dini. Na tunazichambua Aya kwa watu wajuao.
12. Na wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao, na
wakatukana Dini yenu, basi piganeni na waongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana
viapo vya kweli. Huenda (kwa hayo) wakaacha.
13. Je, hamtapigana na watu walio vunja viapo vyao na
wakawa na hamu ya kumfukuza Mtume, nao ndio walio kuanzeni mara ya kwanza? Je,
mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumwogope, ikiwa nyinyi ni
Waumini.
14. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu,
na awahizi na akunusuruni muwashinde, na avipoze vifua vya kaumu ya Waumini,
15. Na aondoe hasira ya nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu
humkubalia toba ya amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
16. Je, mlidhani kuwa mtaachwa tu, bila ya Mwenyezi Mungu
kuwajuulisha wale walio pigana Jihadi kati yenu, na wala hawakumfanya mwendani
wao isipo kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini wenziwe? Na Mwenyezi
Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
17. Haiwi kuwa makafiri ndio waamirishe misikiti ya
Mwenyezi Mungu, hali wanajishuhudishia wenyewe ukafiri. Hao ndio ambao vitendo
vyao vimeharibika, na katika Moto watadumu.
18. Hakika wanao amirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni
wale wanao muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika Sala, na
wakatoa Zaka, na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa
katika waongofu.
19. Je, mnafanya kuwanywesha maji Mahujaji na kuamirisha
Msikiti Mtakatifu ni sawa na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya
Mwisho, na akapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa mbele ya
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
20. Wale walio amini, na wakahama, na wakapigana Jihadi
katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wana cheo kikubwa
zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu.
21. Mola wao Mlezi anawabashiria rehema zitokazo kwake, na
radhi, na Bustani ambazo humo watapata neema za kudumu.
22. Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu yapo
malipo makubwa.
23. Enyi mlio amini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu
kuwa vipenzi vyenu ikiwa wanastahabu ukafiri kuliko Imani. Na katika nyinyi
atakaye wafanya hao ndio vipenzi vyake, basi hao ndio madhaalimu.
24. Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na
wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika,
na majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume
wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri
yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
25. Hakika Mwenyezi Mungu amekunusuruni katika mapigano
mengi, na siku ya Hunayni ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini
haukukufaeni kitu. Na ardhi ikawa dhiki kwenu juu ya upana wake. Kisha mkageuka
mkarudi nyuma.
26. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya
Mtume wake na juu ya Waumini. Na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu
wale walio kufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri.
27. Kisha baada ya hayo Mwenyezi Mungu atawasamehe
awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
28. Enyi mlio amini! Hakika washirikina ni najsi, kwa hivyo
wasiukaribie Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka wao huu. Na ikiwa mnakhofia umasikini,
basi Mwenyezi Mungu atakutajirisheni kwa fadhila yake akipenda. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
29. Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya
Mwisho, wala hawaharimishi alivyo harimisha Mwenyezi Mungu na Mtume, wala
hawashiki Dini ya Haki, miongoni mwa walio pewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa
khiari yao, hali wamet'ii.
30. Na Mayahudi wanasema: Uzeir ni mwana wa Mungu. Na
Wakristo wanasema: Masihi ni mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa
vyao. Wanayaiga maneno ya walio kufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize!
Wanageuzwa namna gani hawa!
31. Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi
badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipo
kuwa wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na
hayo wanayo mshirikisha nayo.
32. Wanataka kuizima Nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa
vyao, na Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize Nuru yake ijapo kuwa makafiri
watachukia.
33. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini
ya Haki ipate kushinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
34. Enyi mlio amini! Hakika wengi katika makuhani na
wamonaki wanakula mali za watu kwa baat'ili na wanazuilia Njia ya Mwenyezi
Mungu. Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya
Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.
35. Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na
kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa:
Haya ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika.
36. Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi
na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo
ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na
washirikina wote kama wao wnavyo pigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi
Mungu yu pamoja na wachamngu.
37. Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni kuzidi katika
kukufuru; kwa hayo hupotezwa walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na
kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyo
itukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo huhalalisha alivyo viharimisha Mwenyezi
Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
makafiri.
38. Enyi mlio amini! Mna nini mnapo ambiwa: Nendeni katika
Njia ya Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia maisha ya
dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na ya
Akhera ni chache.
39. Kama hamwendi atakuadhibuni adhabu chungu, na atawaleta
watu wengine, wala nyinyi hamtamdhuru chochote. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa
kila kitu.
40. Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu
alikwisha mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili
walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika
Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na
akamuunga mkono kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la walio kufuru
kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye
Mwenye nguvu Mwenye hikima.
41. Nendeni mtoke, mkiwa wepesi na wazito, na piganeni
Jihadi kwa mali yenu na nafsi zenu katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Haya ni kheri
kwenu mkiwa mnajua.
42. Na lau ingeli kuwa ipo faida ya papo kwa papo, na
safari yenyewe ni fupi, wangeli kufuata. Lakini wameona ni mbali na kuna
mashaka. Nao wataapa kwa Mwenyezi Mungu: Tungeli weza bila ya shaka tungeli
toka pamoja nanyi. Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa
hakika hao ni waongo.
43. Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini ukawapa ruhusa kabla
ya kubainikia kwako wanao sema kweli, na ukawajua waongo?
44. Hawatakuomba ruhusa wale wanao muamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho, wasende kupigana Jihadi kwa mali yao na nafsi zao. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua wachamngu.
45. Wasio muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na nyoyo
zao zikatia shaka, hao tu ndio wanao kutaka ruhusa. Basi hao wanataradadi
katika shaka zao.
46. Na ingeli kuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka
wangeli jiandalia maandalio, lakini Mwenyezi Mungu kachukia kutoka kwao, na kwa
hivyo akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!
47. Lau wangeli toka nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko,
na wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni mwenu wapo wanao
wasikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
48. Tangu zamani walitaka kukutilieni fitna, na
wakakupindulia mambo juu chini, mpaka ikaja Haki na ikadhihirika amri ya
Mwenyezi Mungu, na wao wamechukia.
49. Na miongoni mwao wapo wanao sema: Niruhusu wala
usinitie katika fitina. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina.
Na hakika Jahannamu imewazunguka.
50. Ukikupata wema unawachukiza, na ukikusibu msiba, wao
husema: Sisi tuliangalia mambo yetu vizuri tangu kwanza. Na hugeuka kwenda zao
nao wamefurahi.
|