10. SURAT YUNUS
(Imeteremka
Makka)
Sura
hii ya Makka imeteremka Makka, na ina Aya 109. Imeanzia kuashiria cheo cha Kitabu
hiki Kitukufu, na wasemayo washirikina yaliyo mkhusu Nabii s.a.w. Kisha ikataja
ulimwengu na ishara za Mwenyezi Mungu Mtukufu ziliomo humo, na malipo ya Siku
ya Kiyama, na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwatendea makafiri, na
kuwakemea kwake kwa hizo itikadi zao, na hali ya watu wakati wa shida na neema,
na uwezo wa Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu, na kuemewa masanamu kufanya
lolote. Na katika Sura hii wanatakiwa kama wanaweza makafiri walete Sura japo
moja ya kuzua. Na pia ndani yake kuna vitisho vikali vya adhabu ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu, na hali za nafsi za watu, na vipi Mwenyezi Mungu anavyo
vichunguza vitendo vyao. Kisha baada ya hayo ikaingia kumwondolea Nabii s.a.w.
kuungulika kwake kwa ukafiri wao, pamoja na kutoa hoja ya kuwavunja kabisa, na
ikampoza kwa kumtajia hadithi za Manabii wengine na kaumu zao. Ikaja hadithi ya
Nuhu, na hadithi ya Musa na Harun na Firauni na Wana wa Israili; kisha
ikaashiriwa hadithi ya Yunus, na kwa jina hilo Sura hii ikaitwa. Na mwisho
ikaelekea Sura hii kubainisha mambo ya Mtume huyu ili kutimiza mawaidha na
mazingatio.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|