1 - 50
1. Alif
Lam Ra. Hizo ni Aya za Kitabu chenye Hikima.
2. Je!
Imekuwa ajabu kwa watu kwamba tumemfunulia mmoja wao kuwa: Waonye watu, na
wabashirie wale walio amini ya kuwa watakuwa na cheo cha juu kwa Mola wao
Mlezi? Wakasema makafiri: Hakika huyu ni mchawi dhaahiri!
3. Hakika
Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, ambaye ameziumba mbingu na ardhi kwa siku
sita, na ametawala kwenye ufalme wake, anaendesha mambo yote. Hapana mwombezi
ila baada ya idhini yake. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Basi
muabuduni Yeye. Je! Hamkumbuki?
4. Kwake Yeye tu ndio marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi ya
Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika Yeye ndiye aliye anzisha uumbaji, na
kisha ataurejesha ili awalipe kwa uadilifu wale walio amini na wakatenda mema.
Na walio kufuru, wao watapata vinywaji vinavyo chemka, na adhabu chungu kwa
sababu ya walivyo kuwa wakikufuru.
5. Yeye ndiye aliye lijaalia jua kuwa na mwangaza, na mwezi
ukawa na nuru, na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu. Mwenyezi
Mungu hakuviumba hivyo ila kwa Haki. Anazipambanua Ishara kwa watu wanao jua.
6. Hakika katika kukhitalifiana usiku na mchana, na katika
alivyo umba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi, zipo Ishara kwa watu wanao
mcha-Mngu.
7. Hakika wasio taraji kukutana nasi, na wakaridhia maisha
ya dunia na wakatua nayo, na walio ghafilika na Ishara zetu,
8. Hao, makaazi yao ni Motoni kwa sababu ya waliyo kuwa
wakiyachuma.
9. Hakika walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi
atawaongoa kwa sababu ya Imani yao. Itakuwa inapita mito kati yao katika
Mabustani yenye neema.
10. Wito wao humo utakuwa: Subhanaka Llahumma
"Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu!" Na maamkio yao humo ni
"Salama". Na mwisho wa wito wao ni: Alhamdulillahi Rabbil A'lamiin
"Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu
wote."
11. Na lau kama Mwenyezi Mungu angeli wafanyia watu haraka
kuwaletea shari kama wanavyo jihimizia kuletewa kheri, bila ya shaka wangelisha
timiziwa ajali yao. Lakini tunawaacha wale wasio tumainia kukutana nasi
wakihangaika katika upotovu wao.
12. Na mtu akiguswa na shida hutuomba naye kaegesha ubavu,
au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama kwamba
hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyo mpata. Ndio namna hiyo wamepambiwa
warukao mipaka yale waliyo kuwa wakiyatenda.
13. Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza kaumu za kabla yenu
walipo dhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa Ishara zilizo wazi; lakini hawakuwa
wenye kuamini. Ndio kama hivyo tunavyo walipa watu wakosefu.
14. Kisha tukakufanyeni nyiye ndio wenye kushika mahala pao
baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyo tenda.
15. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, wale wasio
taraji kukutana na Sisi husema: Lete Qur'ani isiyo kuwa hii, au ibadilishe.
Sema: Hainifalii mimi kuibadilisha kwa nitakavyo nafsi yangu. Mimi sifuati ila
ninayo funuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa, nikimuasi Mola wangu Mlezi,
adhabu ya Siku iliyo kuu.
16. Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli kusomeeni,
wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nalikwisha kaa nanyi umri mzima kabla yake! Basi, je! Hamzingatii?
17. Basi ni nani
aliye dhaalimu zaidi kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu na
akazikanusha Ishara zake? Hakika hawafanikiwi wakosefu.
18. Nao, badala ya
Mwenyezi Mungu, wanaabudu wasio wadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema: Hawa
ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu! Sema: Je! Mnamwambia Mwenyezi Mungu
asiyo yajua ya katika mbingu wala katika ardhi? Subhanahu wa Taa'la!
Ametakasika na ametukuka na hao wanao mshirikisha naye.
19. Wala watu
hawakuwa ila Umma mmoja tu. Kisha wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo
kwisha tangulia kutokana na Mola wako Mlezi, hapana shaka hukumu ingeli kwisha
katwa baina yao katika hayo wanayo khitalifiana.
20. Na wanasema:
Kwa nini hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Mambo ya
ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu. Basi nyinyi ngojeni, na mimi ni pamoja nanyi
katika wanao ngojea.
21. Na tunapo
waonjesha watu rehema baada ya shida waliyo ipata, utawaona wana vitimbi
kuzipangia Ishara zetu. Sema: Mwenyezi Mungu ni Mwepesi zaidi wa kupanga.
Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayo yapanga.
22. Yeye ndiye
anaye kuendesheni bara na baharini. Hata mnapo kuwa majahazini na yakawa
yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, upepo mkali ukawazukia, na
yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakaona wamesha zongwa, basi hapo
humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia niya: Ukituokoa na haya bila ya shaka
tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
23. Lakini
akisha waokoa, mara wanafanya jeuri tena katika nchi bila ya haki. Enyi watu!
Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Hii ni starehe ya maisha ya dunia tu.
Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
24. Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyo
yateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi wanayo ila
watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipo kamilika uzuri wake, na ikapambika, na
wenyewe wakadhani wamesha iweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana,
tukaifanya kama iliyo fyekwa - kama kwamba haikuwapo jana. Namna hivi
tunazipambanua Ishara zetu kwa watu wanao fikiri.
25. Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea Nyumba ya Amani, na
anamwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
26. Kwa wafanyao wema ni wema na zaidi. Wala vumbi
halitawafunika nyuso zao, wala madhila. Hao ndio watu wa Peponi. Humo watadumu.
27. Na
wale walio chuma maovu, malipo ya uovu ni mfano wake vile vile, na yatawafika
madhila. Hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu. Nyuso zao kama kwamba
zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio watu wa Motoni, wao humo
watadumu.
28. Na
siku tutakapo wakusanya wote, kisha tutawaambia walio shirikisha: Simameni
mahali penu nyinyi na wale mlio wafanya washirika. Kisha tutawatenga
baina yao. Na hao walio washirikisha watasema: Nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi.
29. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina yetu na
nyinyi. Hakika sisi tulikuwa hatuna khabari ya ibada yenu.
30. Huko kila mtu atayajua aliyo yatanguliza. Na
watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki, na yote waliyo kuwa
wakiyazua yatawapotea.
31. Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na
kwenye ardhi? Au ni nani anaye miliki kusikia na kuona? Na nani amtoaye hai
kutoka maiti, na akamtoa maiti kutoka aliye hai? Na nani anaye yadabiri mambo
yote? Watasema: Allah, Mwenyezi Mungu. Basi sema: Je! Hamchi?
32. Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu wa
haki. Na kipo kitu gani baada ya haki, isipokuwa upotovu tu? Basi huwaje
mkageuzwa?
33. Ndio kama hivyo kauli ya Mola wako Mlezi itakavyo
wathibitikia wale walio potoka, ya kwamba hawatoamini.
34. Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina aliye
anzisha kuumba viumbe, na kisha akavirejesha? Huwaje, basi, mkadanganywa?
35. Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina anaye
ongoa kwendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi, je, anaye
stahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye ongoa ila
aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?
36. Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana haifai kitu
mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua yote wanayo yatenda.
37. Na haiwezekani Qur'ani hii kuwa imetungwa na haitoki
kwa Mwenyezi Mungu. Lakini hii inasadikisha yaliyo tangulia, na ni mfafanuo wa
Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kutokana na Mola Mlezi wa viumbe vyote.
38. Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura moja
mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipo kuwa Mwenyezi Mungu,
ikiwa nyinyi mnasema kweli.
39.Bali wameyakanusha wasio yaelewa ilimu yake kabla
hayajawajia maelezo yake. Kadhaalika walio kabla yao walikanusha vile vile.
Basi angalia jinsi ulivyo kuwa mwisho wa madhaalimu hao.
40. Na miongoni mwao wapo wanao iamini, na miongoni mwao
wapo wasio iamini. Na Mola wako Mlezi anawajua vyema mafisadi.
41. Na wakikukanusha wewe, sema: Mimi nina a'mali yangu, na
nyinyi mna a'mali yenu. Nyinyi hamna jukumu kwa niyatendayo, wala mimi sina
jukumu kwa myatendayo.
42. Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza. Je, wewe
unaweza kuwafanya viziwi wasikie ijapo kuwa hawafahamu?
43. Na wapo miongoni mwao wanao kutazama. Je, wewe
utawaongoa vipofu ingawa hawaoni?
44. Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu kitu chochote;
lakini watu wenyewe wanajidhulumu nafsi zao.
45. Na Siku atakapo wakusanya, itakuwa kama kwamba
hawakukaa ila saa moja tu ya mchana! Watatambuana. Hakika wamekhasirika walio
kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.
46. Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayo
waahidi, au tukakufisha kabla yake, marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu
ni Shahidi wa wanayo yafanya.
47. Na kila umma una Mtume. Alipo wajia Mtume wao
walihukumiwa baina yao kwa uadilifu, wala hawakudhulumiwa.
48. Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli?
49. Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala kheri ila apendavyo
Mwenyezi Mungu. Kila umma una muda wao walio wekewa. Ukifika muda wao hawakawii
hata saa moja wala hawatangulii.
50. Sema: Mwaonaje ikikufikieni hiyo adhabu yake usiku au
mchana, sehemu gani ya adhabu wanaihimiza wakosefu?
|