101 - 122
101. Na Sisi hatukuwadhulumu, lakini wao wenyewe
wamejidhulumu. Na miungu yao waliyo kuwa wakiiomba badala ya Mwenyezi Mungu
haikuwafaa kitu ilipo kuja amri ya Mola wako Mlezi. Na hiyo miungu
haikuwazidishia ila maangamizo tu.
102. Na ndio kama hivyo ndivyo inavyo kuwa Mola wako Mlezi
anapo ikamata miji inapo kuwa imedhulumu. Hakika mkamato wake ni mchungu na
mkali.
103. Hakika katika haya ipo ishara kwa yule anaye ogopa
adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo Siku itakayo kusanyiwa watu, na hiyo ndiyo Siku
itakayo shuhudiwa.
104. Na Sisi hatuiakhirishi ila kwa muda unao hisabiwa.
105. Siku hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila
kwa idhini yake Mwenyezi Mungu. Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye
furaha.
106. Ama wale wa mashakani hao watakuwamo Motoni
wakiyayayatika na kukoroma.
107. Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo
kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hakika Mola wako Mlezi hutenda apendavyo.
108. Na ama wale walio bahatika, wao watakuwamo Peponi
wakidumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako
Mlezi. Hicho ni kipawa kisio na ukomo.
109. Basi usiwe na shaka juu ya wanayo yaabudu hao.
Hawaabudu ila kama walivyo abudu baba zao zamani. Na hakika Sisi
tutawatimilizia fungu lao bila ya kupunguzwa.
110. Na kwa yakini tulimpa Musa Kitabu; zikazuka khitilafu
ndani yake. Na lau kuwa si neno lilio kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako
Mlezi, bila ya shaka ingeli hukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka
juu yake inayo wahangaisha.
111. Na hakika Mola wako Mlezi atawatimilizia malipo ya
vitendo vyao. Hakika Yeye
anayo khabari ya wayatendayo.
112. Basi,
simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa Mwenyezi
Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo.
113. Wala
msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi
badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa.
114. Na
shika Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na
mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka.
115. Na subiri, kwani Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa
wanao fanya wema.
116. Basi mbona hawakuwamo katika watu wa kabla yenu wenye
vyeo na wasaa wanao kataza uharibifu katika nchi, isipo kuwa wachache tu, ambao
ndio tulio waokoa? Na walio dhulumu walifuata starehe zao, na wakawa ni
wakosefu.
117. Wala hakuwa Mola wako Mlezi wa kuihiliki miji kwa dhulma
tu na hali watu wake ni watenda mema.
118. Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote
wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana,
119. Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na
kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi:
Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja.
120. Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni
ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na
ukumbusho kwa Waumini.
121. Na waambie wale wasio amini: Fanyeni muwezavyo, nasi
pia tunafanya.
122. Na ngojeni, na sisi tunangoja.
123. Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika
ardhi na mbingu, na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na
umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda.
|