12. SURAT YUSUF
(Imeteremka
Makka)
Sura
hii ni ya Makka, na Aya zake ni mia na kumi na moja. Ndani yake Mwenyezi Mungu
amesimulia hadithi ya Yusuf katika Aya tisiini na nane, na ameitangulizia kwa
Aya tatu alizo taja ndani yake huu ufunuo alio mteremshia Muhammad, rehema za
Mwenyezi Mungu na amani zishuke juu yake. Na ameuita ufunuo huu katika Aya ya
kwanza: Kitabu kinacho bainisha. Na katika Aya ya pili akauiita: Qur'ani kwa
Kiarabu, kuwa ni kuashiria kwamba ni haki yake uhifadhiwe kwa maandishi na
katika vifua vya watu vile vile. Kisha katika Aya ya tatu akataja kuwa ufunuo
huu umekusanya simulizi nzuri kabisa, na ukataja kuwa Nabii Muhammad hakuwa
akiyajua hayo kabla hakuteremshiwa huo Wahyi (ufunuo). Na hiyo ni dalili kuwa
haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kisa hichi na Sura hii imemalizikia
kwa kutilia mkazo yaliyo anzia. Na akamuelekeza Nabii mnamo Aya kumi azingatie
kuwa masimulizi haya ni katika khabari za ghaibu, ambazo yeye Nabii, Salla
Llahu alayhi wasallama, hakuwa akizijua, na kuzijua ukweli wake zilivyo, kabla
ya kuteremshiwa Wahyi. Wala yeye hakuwa pamoja na hao ndugu zake Yusuf walipo
kuwa wakipanga mipango yao, na wakiunda njama zao za shari kumuundia ndugu yao
kwa baba. Kisha Qur'ani inamwambia Mtume kuwa inda na husda huwapelekea watu
wengi kuingia ukafirini. Na kwamba pupa yake Mtume s.a.w. kuwa waamini wengi
wao haitomfalia kitu, lakini Qur'ani inampoza kwa hayo kwa kuwa yeye hataki
ujira, ila ni kuwa yeye anawaletea Qur'ani iwe ni uwongofu na ukumbusho kwa
watu wote. Na mwisho wa Sura inaashiria Mitume ambao hadithi zao zimesimuliwa,
na ukasimuliwa msimamo wa kaumu zao, na vipi mwishoe walivyo washinda makafiri
wakosefu. Na katika hadithi hizi za Manabii pana mazingatio kwa wenye akili.
Hakika hii Qur'ani inayo simulia masimulio haya na mengineyo si kitu cha
kutungwa tu na kuzuliwa kuwa kinatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa uwongo. Hakika hii
ni haki na kweli tupu, na hichi ni Kitabu kinacho sadikisha Vitabu sahihi vilivyo
toka mbinguni, na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao zingatia na wakaamini.
Linalo onekana wazi katika sifa za Sura hii ni kuwa kimesimuliwa kisa cha Yusuf
kwa ukamilifu wake. Na pia imeonekana kuwa katika ule ule ukoo mmoja upo
uhasidi ulio enea na pia katika baadhi yao yapo mapenzi. Husda ya wana wa
Yaaqub iliwapelekea kumtumbukiza ndugu yao kisimani. Lakini Mwenyezi Mungu
alimlinda na vitimbi vyao, kama alivyo mkinga na matamanio ya mke wa Mheshimiwa
pale Yusuf alipo fikilia utuuzima nyumbani kwa Mheshimiwa. Mwenyezi Mungu
akamweka vizuri katika nchi ya Misri, na akamjaalia kuwa nchi hiyo iwe
makimbilio (mategemeo) ya wale walio mpangia njama za kumdhuru. Basi ni hivyo
shani yake Subhanahu wa Taa'la kwa Manabii wake na vipenzi vyake. Huwanusuru dhidi
ya maadui zao, na huwathibitisha na kuwaweka vyema katika ardhi maadamu
wanaishika Haki na wanaiamini, na wanaishikilia kamba ya Mwenyezi Mungu.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|