51 - 100
51. Mfalme alisema: Mlikuwa mna nini mlipo mtaka Yusuf
kinyume na nafsi yake? Wakasema: Hasha Lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote
kwake. Mke wa Mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliye mtaka
kinyume na nafsi yake, na hakika yeye ni katika wakweli.
52. Hayo ni apate kujua ya kwamba mimi sikumfanyia khiyana
nyuma yake; na ya kwamba Mwenyezi Mungu haziongoi hila za makhaini.
53. NAMI sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno
kuamrisha maovu, isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika
Mola wangu Mlezi ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
54. Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu mwenyewe
khasa. Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani kwetu na
umeaminika.
55. Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani
hakika mimi ni mlinzi mjuzi.
56. Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa
humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo
ya wafanyao mema.
57. Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio
amini na wakawa wachamngu.
58. Wakaja ndugu zake Yusuf, na wakaingia kwake. Yeye
akawajua na wao hawakumjua.
59. Na alipo watengenezea tayari haja yao alisema:
Nileteeni ndugu yenu kwa baba. Je! Hamwoni ya kwamba mimi ninatimiza kipimo,
nami ni mbora wa kukirimu?
60. Na msipo niletea basi hampati kipimo chochote kwangu,
wala msinikurubie.
61. Wakasema: Sisi tutamrairai baba yake; na bila ya shaka
tutafanya hayo.
62. Na Yusuf akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao
katika mizigo yao, ili wazione watakapo rudi kwa watu wao wapate kurejea tena.
63. Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba
yetu! Tumenyimwa chakula zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate
kupimiwa; na yakini sisi tutamlinda.
64. Je, nikuaminini kwa huyu ila kama nilivyo kuaminini kwa
nduguye zamani? Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kulinda, naye ndiye Mbora
wa kurehemu kuliko wenye kurehemu wote.
65. Na walipo fungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao
wamerudishiwa. Wakasema: Ewe
baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Wacha
tuwaletee watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na tutaongeza shehena ya
ngamia. Na hicho ni kipimo kidogo.
66. Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa
Mwenyezi Mungu kwamba lazima mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi
walipo mpa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo.
67. Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali
ingieni kwa milango mbali mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi
Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea,
na juu yake Yeye wategemee wanao tegemea.
68. Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao,
haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika nafsi
ya Yaa'qub aliitimiza. Na hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu
tulimfundisha; lakini watu wengi hawajui.
69.Na walipo ingia kwa Yusuf alimchukua nduguye akasema:
Mimi hakika ni nduguyo. Basi usihuzunike kwa waliyo kuwa wakiyafanya .
70. Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia
kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi
wasafiri! Hapana shaka nyinyi ni wezi!
71. Wakasema nao wamewakabili: Kwani mmepoteza nini?
72. Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na ataye lileta
atapewa shehena nzima ya ngamia. Nami ni dhaamini wa hayo.
73.
Wakasema: Wallahi! Mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika
nchi hii, wala sisi si wezi.
74.
Wakasema: Basi malipo yake yatakuwa nini ikiwa nyinyi ni waongo?
75.
Wakasema: Malipo yake ni yule ambaye ataonekana nalo yeye huyo ndiye malipo
yake. Hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
76. Basi
akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akakitoa katika mzigo
wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye kwa
sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye
vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi.
77.
Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba zamani. Lakini Yusuf
aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha. Akawaambia: Nyinyi mko katika
hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayo singizia.
78.
Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Huyu anaye baba mzee sana. Kwa hivyo mchukue mmoja
wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.
79.
Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumshika yeyote yule isipo kuwa tuliye
mkuta naye kitu chetu. Hivyo basi tutakuwa wenye kudhulumu.
80. Walipo
kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu
amechukua ahadi kwenu kutokana na Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo mlimkosa
katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi mimi sitotoka nchi hii mpaka baba yangu
anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu.
81. Rudini kwa
baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Mwanao ameiba. Na sisi hatutoi ushahidi
ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu.
82. Na waulize
watu wa mji tulio kuwako, na msafara tulio kuja nao. Na hakika sisi
tunasema kweli.
83. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo
fulani. Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika
Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
84. Naye akajitenga nao, na akasema: Ah! Masikini Yusuf! Na
macho yake yakawa meupe kwa huzuni aliyo kuwa akiizuia.
85.
Wakasema: Wallahi! Huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au uwe katika
walio hiliki.
86.
Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu sikitiko langu na huzuni yangu.
Na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.
87. Enyi
wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji ya
Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa
watu makafiri.
88. Basi
walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata shida, sisi
na watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi tupimie kipimo na fanya kama
unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka.
89. Akasema: Je!
Mmejua mliyo mfanyia Yusuf na nduguye mlipo kuwa wajinga?
90. Wakasema:
Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu.
Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anaye mcha Mungu na akasubiri, basi
Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa wafanyao mema.
91.
Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi, na hakika
sisi tulikuwa wenye kukosa.
92.
Akasema: Leo hapana lawama juu yenu. Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni
Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu.
93.
Nendeni na kanzu yangu hii na mumwekee usoni baba yangu, atakuwa mwenye kuona.
Na mje nao watu wenu wote wa nyumbani.
94. Na
ulipo ondoka tu msafara baba yao alisema: Hakika mimi nasikia harufu ya Yusuf,
lau kuwa hamtanituhumu.
95.
Wakasema: Wallahi! Hakika bado ungali katika upotovu wako wa zamani.
96. Basi
alipo fika mbashiri na akaiweka kanzu usoni pake alirejea kuona. Akasema: Je!
Sikukwambieni kuwa mimi najua ya Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi?
97.
Wakasema: Ee baba yetu! Tuombee msamaha kwa dhambi zetu. Hapana shaka sisi
tulikuwa na makosa.
98.
Akasema: Nitakuja kuombeeni msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye
Mwenye maghfira na Mwenye kusamehe.
99. Na
walipo ingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema: Ingieni Misri,
Inshallah, mmo katika amani.
100. Na
akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka
kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto
yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi Mungu
amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya
Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole
kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
|