15. SURATUL HIJR
(Imeteremka
Makka)
Suratul
Hijr ni Sura ya Makka. Nayo ina Aya 99. Imeanza kwa harufi za kutamkwa
zenye kueleza kwamba Qur'ani imejengeka kwa harufi hizi hizi mnazo zitumia
katika maneno yenu, na juu ya hivyo ni Muujiza kwenu, hamwezi kuleta kama hii.
Kwani aliye iteremsha ni Mwenyezi Mungu, Aliye takasaika, na Akatukuka. Na hizo
harufi pia ni kama kuwazindua wale wanao ipuuza Qur'ani, inawalingania,
inawaita, waisikilize. Asaa wakanufaika, na wakahidika kumfuata Mwenyezi Mungu.
Sura hii tukufu inabainisha ili watu wazingatie yaliyo wapata kaumu zilizo
tangulia, na khabari za Manabii walio kwisha pita, na yaliyo wapata kutokana na
watu wao. Na pia Sura hii inaonyesha ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu,
katika mbingu zilizo nyanyuliwa na zenye sayari ziilizo hifadhiwa, na ardhi
iliyo tandikwa, na kukunjuliwa, na milima iliyo simama imara, na pepo zenye
kubeba maji, na zenye kupandishia miti. Na Sura hii pia inaashiria mpambano wa
mwanzo katika maumbile ya asli baina ya maluuni Iblisi na Adam na mkewe, na
kuendelea mpambano huo baina ya kheri na shari mpaka imalizike dunia. Kisha
tena malipo ya shari Siku ya Kiyama, na malipo ya kheri. Na baada ya hayo
Mwenyezi Mungu anasimulia visa vya Manabii wawili, Ibrahim na Luut'i, na watu
wa Al Hijr. Na Sura inaeleza cheo cha Qur'ani, na hali ya washirikina katika
kuipokea, na impasavyo Nabii kwa mnasaba wa ukafiri wao, navyo ni kufikisha
ujumbe wake, na kuutangaza, na kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka ifike amri ya
yakini.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|