16. SUURAT AN NAH'L
(Imeteremka
Makka)
Sura
hii ni ya Makka, isipo kuwa Aya tatu za mwisho. Hizo ni za Madina. Idadi
ya Aya zake ni mia na ishirini na nane. Sura hii tukufu imeanzia kutilia mkazo
maonyo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa washirikina, na kubainisha uwezo wake
Subhanahu wa Taa'la katika kutimiza ahadi hiyo, kwa dalili ya kuumba kwake
mbingu na ardhi. Kisha kawabainishia watu wote kumuumba kwake ngamia, na
kuotesha kwake makulima, na aliyo yaumba baharini, kama samaki wa kuliwa, na
majohari ya mapambo. Kisha akaashiria yanayo wajibikia kwa neema hizo, nayo ni
kumshukuru Subhanahu, na waajibu wa kumuabudu Yeye peke yake, na kuwakabili
washirikina kwa kuwaita watambue Upweke wa Mwenyezi Mungu; na imetaja uzushi wa
washirikina kuizulia , na kudai kuwa hiyo ni hadithi za uwongo za kale. Kisha
Subhanahu ameashiria adhabu ya washirikina Siku ya Kiyama na starehe za
Waumini. Baadaye Subhanahu akataja kukanya kwa washirikina kukhusu kufufuliwa
na kushikilia kwao kukanya. Naye Subhanahu anapinga ukafiri wao kwa kubainisha
uwezo wake, na anatilia mkazo ahadi yake kwa wachamngu na vitisho vyake kwa
makafiri. Kisha anakaribisha kufufuliwa kwa kueleza uwezo wake juu yao, na kuwa
viumbe vyote vinamnynyekea Yeye Aliye takasika, na anabainisha kuwa ni Yeye
Subhanahu ndiye anaye kashifu. Na anabainisha upotovu wa washirikina katika
itikadi yao kuamini vitu visivyo weza kuleta nafuu wala madhara, na uovu wa
maoni yao kwa wanawake wote, watoto na watu wazima. Naye Subhanahu ameashiria
khabari za Mitume walio tangulia, akataka tuuzingatie uumbaji wake wa vitu na
faida ziliomo ndani yake kwa ajili ya watu, na kutafautiana riziki, kuwa
matajiri wanapewa zaidi kuliko masikini, na neema zake kwa watu kuwa wengine
wanaume na wengine wanawake, na kuzaliana kwa kuoana. Naye Subhanahu akaingia
kupiga mifano ili kueleza kudra yake. Kisha akataka watu waangalie vipi ubora
wa kuumba unavyo onyesha ubora wa Mwenye kuumba na kuenea neema zake. Na vipi
washirikina wanavyo zipinga neema hizi tukufu. Na baada ya kueleza matakwa ya
Uislamu kuleta uadilifu, na kuunganisha udugu kwa kutimiza ahadi, na muujiza wa
Qur'ani, na ukafiri wa washirikina kuikataa Qur'ani, na kuizulia uwongo, Aliye
takasika ameashiria hali ya washirikina Siku ya Kiyama. Amebainisha vipi
walivyo kuwa wakihalalisha na wakiharimisha bila ya hoja. Akaashiria vipi
Mayahudi walivyo wakaribia washirikina, na akabainisha kuwa yapasa wasiadhibiwe
isipo kuwa kwa kadiri ya walivyo tenda, na kuwa ni waajibu wa Waumini wasubiri,
na washikamane na uchamngu na kufanya ihsani.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|