18. SURA AL KAHF
(Imeteremka
Makka)
Sura
hii ni ya Makka, isipo kuwa Aya 38, na Aya zinazo anzia 83 mpaka 101. Basi
zimo Aya ishirini za Madina. Nayo imeanzia kwa kumhimidi Mwenyezi Mungu Mtukufu
kwa kuiteremsha , na kubainisha kuwa Qur'ani ni onyo na bishara. Ndani yake
lipo onyo kwa wanao dai kuwa ati Mwenyezi Mungu ana mwana. Na humu imetajwa
hamu kubwa aliyo nayo Nabii ya kutaka waamini wale anao waita kwenye mlingano
wa Mwenyezi Mungu. Kisha kikatajwa kisa cha Ahlil Kahf, Watu wa Pangoni, walio
lala usingizi kisha wakaamka baada ya kukaa katika pango lao muda wa miaka mia
tatu na tena wakazidishiwa tisa. Na watu hao walikuwa Wakristo walio kuwa
wakikimbia udhalimu wa mtawala wa Kirumi. Wakalala katika pango muda huo, kisha
wakaamka ili kuwa ni ishara ya uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kufufua baada ya
kufa.
Kisha baada ya hayo Mwenyezi Mungu akamuamrisha kusoma Qur'ani na aitumie kwa
kuonya na kubashiri. Kisha imebainishwa hali ya watu wa Peponi na watu wa
Motoni. Na Mwenyezi Mungu akapiga mifano ya watu wawili, mmoja tajiri anajitapa
kwa mali yake na wanawe. Na wa pili anatafakhari kwa Mwenyezi Mungu wake. Na
amebainisha Subhanahu kuwa ulinzi wake ndio wa Haki. Na tena Subhanahu ameeleza
starehe ya duniani inayo pita, na neema ya daima au adhabu chungu ya Siku ya
Kiyama. Tena Subhanahu ametaja hadithi ya Musa pamoja na Mja Mwema aliye pewa
ilimu kutokana na Mwenyezi Mungu. Na katika kisa hichi inapatikana sura ya vipi
mtu anaweza asijue mambo, hata akiwa Nabii Mtume katika Mitume imara - Ulul
a'zmi - kwa kudra yake Mwenyezi Mungu, ila akiwa Yeye Mwenyezi Mungu
akimjuulisha. Tena anatajwa Dhul-qarnaini na kufika kwake mashariki ya mbali,
na alivyo jenga Ukuta. Kisha yatakayo kuwa Siku ya Kiyama, na malipo ya
Waumini, na ilimu ya Mwenyezi Mungu na maneno yake yasiyo malizika. Na Sura
ikakhitimishia kwa kueleza Njia ya Kumridhi Subhanahu.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|