51 - 100
51. Sikuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wala kuumbwa
kwa nafsi zao. Wala sikuwafanya wapotezao kuwa ni wasaidizi.
52. Na siku atakapo sema (Mwenyezi Mungu): Waiteni hao mlio
dai kuwa ni washirika wangu. Basi watawaita, na wao hawato waitikia. Nasi
tutaweka baina yao maangamio.
53. Na wakhalifu watauona Moto na watajua ya kwamba wao
lazima wataingia humo; wala hawatapata pa kuuepuka.
54. Na bila ya shaka tumewaelezea watu katika hii Qur'ani
kila namna ya mfano. Lakini mwanaadamu amezidi kuliko kila kitu kwa ubishi.
55. Na hapana kilicho wazuia watu kuamini ulipo wajia
uwongofu na wakaomba maghfira kwa Mola wao Mlezi, isipo kuwa yawafikie ya wale
wa zamani, au iwafikie adhabu jahara.
56. Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na waonyaji. Na
walio kufuru wanabishana kwa uwongo, ili kwa uwongo huo waivunje kweli. Na
wanazifanya Ishara zangu na yale waliyo onywa kuwa ni mzaha.
57. Na ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye
kumbushwa Ishara za Mola wake Mlezi, naye akazipuuza na akasahau yaliyo
tangulizwa na mikono yake? Hakika Sisi tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao ili
wasifahamu, na uziwi kwenye masikio yao. Na ukiwaita kwenye uwongofu hawakubali
kabisa kuongoka.
58. Na Mola wako Mlezi ni Msamehevu Mwenye rehema. Lau
angeli wachukulia kwa mujibu waliyo yachuma, bila ya shaka angeli wafanyia
haraka kuwaadhibu. Lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya
kuepukana nayo.
59. Na miji hiyo tuliwaangamiza watu wake walipo dhulumu.
Na tukawawekea miadi ya maangamizo yao.
60. Na pale Musa alipo mwambia kijana wake: Sitoacha
kuendelea mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda
mrefu.
61. Basi wawili hao walipo fika zinapo kutana hizo bahari
mbili walimsahau samaki wao, naye akashika njia yake kaporonyokea baharini.
62. Walipo kwisha pita alimwambia kijana wake: Tupe chakula
chetu cha mchana. Kwa hakika tumepata machofu kweli kwa hii safari yetu.
63. Akasema (kijana): Waona! Pale tulipo pumzika penye
jabali basi mimi nilimsahau yule samaki. Na hapana aliye nisahaulisha
nisimkumbuke ila Shet'ani tu. Naye akashika njia yake baharini kwa ajabu.
64. (Musa) akasema: Hayo ndiyo tuliyo kuwa tunayataka. Basi
wakarudi nyuma kwa kufuata njia waliyo jia.
65. Basi wakamkuta mja katika waja wangu tuliye mpa rehema
kutoka kwetu, na tukamfunza mafunzo yaliyo toka kwetu.
66. Musa akamwambia: Nikufuate ili unifunze katika ule
uwongofu ulio funzwa wewe?
67. Akasema: Hakika wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja
nami.
68. Na utawezaje kuvumilia yale usiyo yajua vilivyo undani
wake?
69. Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona
mvumilivu, wala sitoasi amri yako.
70. Akasema: Basi ukinifuata usiniulize kitu mpaka mimi
nianze kukutajia.
71. Basi wawili hao wakatoka, hata walipo panda jahazi
(yule mtu) akaitoboa. (Musa) akasema: Unaitoboa uwazamishe watu wake? Hakika
umefanya jambo baya.
72. Akasema: Sikukwambia hutaweza kuvumilia kuwa pamoja
nami?
73. (Musa) akasema: Usinichukulie kwa niliyo sahau, wala
usinipe uzito kwa jambo langu.
74. Basi wakatoka wawili hao mpaka wakamkuta kijana,
akamuuwa. (Musa) akasema: Ala! Umemuuwa mtu asiye na kosa, na wala hakuuwa! Ama
hakika umefanya jambo baya kabisa!
75. AKASEMA: Je!
Sikukwambia kwamba hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami?
76. Akasema:
Nikikuuliza kitu chochote baada ya haya usifuatane nami, kwani umekwisha pata
udhuru kwangu.
77. Basi wakatoka
mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja. Wakawaomba watu wake wawape chakula, nao
wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, (yule mja mwema)
akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli taka ungeli chukua ujira kwa haya.
78. (Yule mtu)
akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Sasa nitakueleza maana ya
yale uliyo kuwa huwezi kuyastahamilia.
79. Ama ile
jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu,
kwani nyuma yao alikuwako mfalme anaghusubu majahazi yote.
80. Na ama yule
kijana, wazazi wake walikuwa ni Waumini. Tukakhofu asije watia mashakani kwa
uasi na ukafiri.
81. Basi
tulitaka Mola wao Mlezi awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa
kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma.
82. Na ama ukuta,
huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako
khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka
wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa
Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya
hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria.
83. Na
wanakuuliza khabari za Dhul- Qarnaini. Waambie: Nitakusimulieni baadhi ya
hadithi yake.
84. Sisi
tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia za kila kitu.
85. Basi akaifuata njia.
86. Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika
checmchem yenye matope meusi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe
Dhul-Qarnaini! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.
87. Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na kisha
atarudishwa kwa Mola wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo juulikana.
88. Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata malipo
mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu.
89. Kisha
akaifuata njia.
90. Hata alipo
fika matokeo ya jua aliliona linawachomozea watu tusio wawekea pazia la
kuwakinga nalo.
91. Ndio
hivyo hivyo. Na Sisi tulizijua vilivyo khabari zake zote.
92. Kisha
akaifuata njia.
93. Hata
alipo fika baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban
hawakuwa wanafahamu lolote.
94.
Wakasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Hakika Juju-wa-maajuju wanafanya uharibifu katika
nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?
95.
Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora zaidi. Lakini nyinyi
nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina yenu na wao.
96. Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi
iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama
moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie.
97. Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa.
98. Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu Mlezi. Na
itapo fika ahadi ya Mola wangu Mlezi atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu
Mlezi ni kweli tu.
99. Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao. Na
baragumu litapulizwa, na wote watakusanywa pamoja.
100. Na siku hiyo tutawadhihirishia wazi Jahannamu makafiri
waione.
|