2. SURA AL- BAQARA
(Imeteremka Madina)
Sura hii imeteremka Madina baada ya Hijra. Nayo
ndiyo sura ndefu kuliko zote katika kwa mujibu wa mtungo wa Msahafu. Sura hii
imeanzia kueleza kwa tafsili yale yaliyo malizikia Sura ya Al Faatiha. Imetaja
kuwa Qur'ani ndiyo msingi wa uwongofu, na imewataja wale walio neemeshwa na
Mwenyezi Mungu kwa kupata radhi zake, na wale walio kasirikiwa, nao ni makafiri
na wanaafiki.
Sura imeeleza ukweli wa Qur'ani, na kwamba wito wake ni wa kweli usio na shaka.
Kisha ikaingia kueleza namna tatu za watu: Waumini, Makafiri na Wanaafiki. Na
ikataja Daa'wa, Mlingano, au Wito, kuwaita watu wamuabudu Mwenyezi Mungu pekee,
na ikawaonya makafiri, na ikawapa bishara njema Waumini. Baadaye ikawaelekea
Wana wa Israili khasa kwa kuwaita na kuwakumbusha siku za Mwenyezi Mungu, na
kwa vituko vyao na Musa a.s. na kuwakumbusha khabari za Ibrahim na Ismail na
walivyo ijenga Al Kaaba. Hayo yamechukua karibu nusu ya Sura. Mazungumzo
yakawageukia Waumini wazingatie yaliyo wapata Mayahudi na Wakristo.
Mazungumzo yakaingia kuwasemeza watu wa Qur'ani kwa kuwakumbusha mambo ambayo
umma wa Musa na umma wa Muhammad walivyo shirikiana katika kutukuzwa Ibrahim na
kuongoka kwake na nasaba yake, na kwa kutaja kibla na mfano wa hayo.
Kisha yakaja mazungumzo juu ya Tawhid (Upweke wa Mwenyezi Mungu) na kukumbusha
Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kumuashiria Yeye. Na yakaja masimulizi juu ya
ushirikina, na juu ya vyakula vilivyo harimishwa, na kwamba kuharimisha na
kuhalalisha ni haki ya Mwenyezi Mungu peke yake.
Sura ikaingia kubainisha misingi ya wema, na kutaja baadhi ya hukumu za Saumu,
na wasia, na kula mali ya watu kwa dhulma, na kisasi, na vita, na Hija, na
ulevi, na kamari, na ndoa na talaka, na kunyonyesha, na eda na mengineyo. Hali
kadhaalika yamezungumzwa mambo ya itikadi kwa jumla kama Utume, Tawhidi,
kufufuliwa. Yametajwa mas-ala ya kutoa sadaka na Zaka, riba, biashara, kuandikiana
madeni. Mwishoe Sura yakhitimisha kwa dua ya Waumini kumwomba Mola wao Mlezi
awanusuru na awasaidie.
Sura hii imekusanya misingi kadhaa wa kadhaa. Miongoni mwayo ni:
Kwamba Njia ya Mwenyezi Mungu na kuishika Dini yake ni dharura kwa ajili ya
kupata mafanakio duniani na Akhera, na kwamba haielekei kwa mwenye akili
kuwaita watu watende mema naye akajisahau mwenyewe; na ya kwamba yapasa
kuchagua kheri kuliko shari, na kukhiari lilio bora kuliko lilio duni.
Na kwamba misingi ya Dini ni mitatu, nayo ni: Kumuamini Mwenyezi Mungu, Kuamini
kufufuliwa, na Kutenda mema.
Na kwamba malipo ni kwa Imani na vitendo pamoja. Shuruti ya Imani ni kukiri kwa
nafsi na kukubali kwa moyo kila alilo kuja nalo Mtume s.a.w., na kwamba wasio
kuwa Waislamu hawatokuwa radhi na Waislamu mpaka Waislamu wafuate dini yao hao
walio potea.
Na kwamba kwa jumla urafiki katika sharia yapasa uwe kwa wenye kushika Imani na
uadilifu, sio kwa watu wa kufuru na dhulma, na kwamba Imani ya Dini ya Mwenyezi
Mungu inalazimisha uwepo umoja na kuwafikiana, na kutofuata hayo huleta
khitilafu na kutengana. Kwa ajili ya kupata mambo makuu inalazimu kutafuta
msaada kwa Subira na Sala. Kufuata kipofu-pofu ni upotovu, na hupelekea ujinga
na chuki za kitaifa.
Na kwamba Mwenyezi Mungu amewahalalishia waja wake vyakula vizuri na
amewaharimishia vichache vilivyo viovu; wala haijuzu kwa asiye kuwa Mwenyezi
Mungu kuhalalisha au kuharimisha kitu. Na vilivyo harimishwa huhalalishiwa
mwenye dharura, kwa sababu dharura huruhusu vilivyo katazwa, na dharura hupimwa
kwa kadiri yake. Dini imejengwa juu ya wepesi na kuondoa mikazo. Kwani Mwenyezi
Mungu hailazimishi nafsi ila kwa kiasi ya uwezo wake, wala hawaamrishi waja
wake ila kwa wanalo liweza. Ni haramu, haijuzu mtu kujipelekea nafsi yake
kwenye maangamizo. Kila jambo hutafutwa kwa sababu zake na njia zake zitakao
fikilia. Kulazimisha katika dini
kunakatazwa. Kupigana vita ni kwa ajili ya kujilinda, na kwa ajili ya kuhifadhi
uhuru wa dini, na kuulinda utukufu wa Uislamu katika miji yake.
Na kwamba Muislamu anayo haki ya kutaka sehemu yake katika dunia, kama anavyo
tekeleza wajibu wake kwa ajili ya Akhera, na kwamba kutimiza haja na kuleta
maslaha ni miongoni mwa makusudio ya Sharia.
Na kwamba Imani na Subira ni sababu mbili zinazo wapelekea wachache walio
waadilifu kuwashinda wengi wenye kudhulumu, na kula mali ya watu kwa upotovu ni
haramu, na mwanaadamu analipwa kwa vitendo vyake mwenyewe si kwa vitendo vya
mwenginewe, na hikima ya utungaji sharia inafahamiwa na akili iliyo kaa sawa kwa
kuwa ndani yake mna haki na uadilifu na maslaha ya waja.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|