20. SURAT T'AHA
(Imeteremka
Makka)
SURA
HII ni ya Makka, isipo kuwa Aya mbili, nazo ni Aya 130 na 131. Hisabu ya Aya zake ni 135. Sura hii
imeanza kwa harufi mbili za kuzindua juu ya muujiza wa Qur'ani, na kuwazindua wasikilizaji
waisikilize. Baada ya harufi hizo mbili cheo cha Qur'ani kimetajwa, na utukufu
wa hii Qur'ani ni utukufu wa Mwenye kuileta, naye ni Mwenyezi Mungu, Subhanahu
wa Taa'la, Mmiliki mbingu na ardhi, Mwenye kujua siri, na kilicho fichikana
kuliko siri. Kisha kimesimuliwa kisa cha Musa a.s. pamoja na Firauni, na vipi
alipo anza kupewa utume Nabii Musa a.s. Na yametajwa maombi yake kutaka nduguye
Harun a.s. awe msaidizi wake wa kumpa nguvu, tena vipi walivyo kutana na
Firauni baada ya kitisho cha mkutano wake kwa ajili ya ujeuri wake. Na katika
mintarafu ya haya Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha kuzuka kwa Musa a.s.
Katika Sura hii pana majibizano baina ya Musa na Firauni, tena baina ya Musa
a.s. na wachawi, na hali ya Musa ya kuogopa kushindwa mbele ya wachawi, na
fimbo yake ilipo zimeza kamba zao, na tena mwisho vipi yalivyo ishia mambo ya
wachawi na kuamini kwao, na Firauni kuwaadhibu. Kisha ikatajwa vipi Musa alivyo
toka yeye na Wana wa Israili kutokana na Firauni, na vipi alivyo zama Firauni,
naye alikuwa kawafuatia baada ya kupasuka bahari; na vipi Musa aliokoka akafika
Jabal T'ur akawaacha watu wake ili ende kwenye mlima kuzungumza na Mola wake
Mlezi. Na Msamaria akawafitini kwa kuwachochea waliabudu sanamu la ndama lililo
undwa kwa dhahabu. Na ilikuwa ukipita upepo ndani yake hutoa sauti. Musa
alikasirika kwa yaliyo tokea, akamkamata kichwa nduguye akimvutia kwake.
Kisha katika Sura hii tukufu yakatokea yaliyo msibu Msamaria. Mwenyezi Mungu
Subhanahu amesimulia hadithi ya kuvuka katika hadithi za Musa na nyenginezo. Na
mwisho wa Sura pana mausio mema juu ya Subira, na Usamehevu, na Sala. Kisha
ikabainishwa kubwatika washirikina katika matakwa yao ya muujiza mwengine usio
huu wa Qur'ani; na Subhanahu ameashiria hikima ya kuwatuma Mitume. Tena Sura
hii tukufu imekhitimisha kwa kuashiria adhabu watakayo pata makafiri, na malipo
mema watakayo pata Waumini.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|