1 - 50
1. T'AHA!
2. Hatukukuteremshia Qur'ani ili upate mashaka.
3. Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea.
4. Materemsho yatokayo kwa aliye umba ardhi na mbingu
zilizo juu.
5. Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliye tawala juu ya Kiti
cha Enzi.
6. Ni vyake vyote viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi,
na viliomo baina yao, na viliomo chini ya ardhi.
7. Na ukinyanyua sauti kwa kusema...basi hakika Yeye anajua
siri na duni kuliko siri.
8.
Mwenyezi Mungu! Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Yeye ana majina mazuri
kabisa.
9. Na je! Imekufikia hadithi ya Musa?
10. Alipo uona moto, akawaambia watu wake: Ngojeni! Mimi
nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga kutoka huo moto, au nikapata
uongofu kwenye moto.
11. Basi alipo ufikia akaitwa: Ewe Musa!
12. Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu
vyako. Kwani upo katika bonde
takatifu la T'uwa.
13. Nami
nimekuteua wewe; basi sikiliza unayo funuliwa.
14. Hakika Mimi
ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na
ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.
15. Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia kuificha,
ili kila nafsi ilipwe kwa iliyo yafanya.
16. Kwa hivyo asikukengeushe nayo yule ambaye haiamini na
akafuata pumbao lake ukaja kuhiliki.
17. Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe
Musa?
18. Akasema: Hii ni fimbo yangu; naiegemea na
ninawaangushia majani kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi
mengine.
19. Akasema: Itupe, ewe Musa!
20. Akaitupa. Mara ikawa nyoka anaye kwenda mbio.
21. Akasema: Ikamate, wala usiogope! Tutairudisha hali yake
ya kwanza.
22. Na uambatishe mkono wako kwenye ubavu. Utatoka mweupe
pasipo kuwa na madhara yoyote. Hiyo ni ishara nyengine.
23. Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa.
24. Nenda kwa Firauni; kwani hakika yeye amepindukia
mipaka.
25. (Musa) akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu,
26. Na unifanyie
nyepesi kazi yangu,
27. Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu,
28. Wapate kufahamu maneno yangu.
29. Na nipe waziri katika watu wangu,
30. Harun,
ndugu yangu.
31. Kwake
yeye niongeze nguvu zangu.
32. Na
umshirikishe katika kazi yangu.
33. Ili tukutakase sana.
34. Na tukukumbuke sana.
35. Hakika Wewe unatuona.
36. Akasema: Hakika Umepewa maombi yako, ewe Musa!
37. Na hakika tulikwisha kufanyia hisani mara nyengine...
38. Pale tulipo mfunulia mama yako yaliyo funuliwa,
39. Ya kuwa mtie katika kisanduku, na kisha kitie mtoni, na
mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua
adui yangu naye ni adui yake. Na nimekutilia mapenzi yanayo tokana kwangu, na
ili ulelewe machoni mwangu.
40. Dada yako
alipo kwenda na akasema: Je! Nikujuulisheni mtu wa kuweza kumlea? Basi
tukakurejesha kwa mama yako ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na
ulimuuwa mtu, nasi tukakuokoa katika dhiki, na tukakujaribu kwa majaribio
mengi. Ukakaa miaka kwa watu wa Madyana. Kisha ukaja kama ilivyo kadiriwa, ewe
Musa!
41. Na
nimekuteuwa kwa ajili ya nafsi yangu.
42. Nenda, wewe
na ndugu yako, pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka.
43. Nendeni kwa
Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka.
44. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.
45. Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa
asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.
46. Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi. Nasikia
na ninaona.
47. Basi mwendeeni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa
Mola wako Mlezi! Basi waache Wana wa Israili watoke nasi, wala usiwaadhibu.
Sisi tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na amani itakuwa juu ya
aliye fuata uwongofu.
48. Hakika tumefunuliwa sisi kwamba hapana shaka adhabu
itamsibu anaye kadhibisha na akapuuza.
49. (Firauni) akasema: Basi Mola wenu Mlezi ni nani, ewe
Musa?
50. Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu
umbo lake, kisha akakiongoa.
|