51 - 100
51. Akasema: Nini hali ya karne za kwanza?
52. Akasema: Ilimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika
Kitabu. Mola wangu Mlezi hapotei wala hasahau.
53. Ambaye amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na
akakupitishieni humo njia, na akakuteremshieni kutoka mbinguni maji. Na kwa
hayo tukatoa namna mbali mbali za mimema.
54. Kuleni, na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo
zipo ishara kwa wenye akili.
55. Kutokana nayo (ardhi) tumekuumbeni, na humo
tunakurudisheni, na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine.
56. Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini
alikadhibisha na akakataa.
57. Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika nchi
yetu kwa uchawi wako?
58. Basi sisi hakika tutakueletea uchawi kama huo. Basi
weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patapo
kuwa sawa.
59. Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu; na watu
wakusanywe kabla ya adhuhuri.
60. Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha
akaja.
61. Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu
uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe!
62. Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe, na
wakanong'ona kwa siri.
63. Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka
kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora
kabisa.
64. Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa
kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakaye shinda.
65. Wakasema:
Ewe Musa! Je! Utatupa wewe, au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa?
66. Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na
fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio.
67. Basi Musa akaingia khofu nafsi yake.
68. Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda.
69. Na
kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika
walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo.
70. Basi
wachawi wakaangushwa wanasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa
Harun na Musa!
71. (Firauni) akasema: Oh! Mnamuamini kabla sijakupeni
ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliye kufundisheni uchawi. Basi kwa
yakini nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na
nitakutundikeni misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua
ni nani katika sisi aliye mkali wa kuadhibu na kuiendeleza adhabu yake.
72. Wakasema: Hatutokukhiari wewe kuliko ishara waziwazi
zilizo tujia, na kuliko yule aliye tuumba. Basi hukumu utavyo hukumu; kwani
wewe unahukumu haya ya maisha ya duniani tu.
73. Hakika sisi tumemuamini Mola wetu Mlezi ili atusamehe
makosa yetu na uchawi ulio tulazimisha kuufanya. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora
na Mwenye kudumu zaidi.
74. Hakika ataye mjia Mola wake Mlezi naye ni mkhalifu,
basi kwa yakini, yake huyo ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi.
75. Na atakaye mjia naye ni Muumini aliye tenda mema, basi
hao ndio wenye vyeo vya juu.
76. Bustani za milele zipitazo mito kati yake, wadumu humo.
Na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa.
77. Na tulimfunulia Musa: Toka usiku na waja wangu, na
uwapigie njia kavu baharini. Usikhofu
kukamatwa, wala usiogope.
78.
Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake. Basi kiliwafudikiza humo baharini
kilicho wafudikiza.
79. Na
Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa.
80. Enyi
Wana wa Israili! Hakika tulikuokoeni na adui yenu, na tukakuahidini upande wa
kulia wa mlima. Na tulikuteremshieni Manna na Salwa.
81. Kuleni katika vitu vizuri hivyo tulivyo kuruzukuni,
wala msiruke mipaka katika hayo, isije ikakushukieni ghadhabu yangu. Na inaye
mshukia ghadhabu yangu basi huyo ameangamia.
82. Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anaye tubia,
na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka.
83. Na nini kilicho kutia haraka ukawaacha watu wako, ewe
Musa?
84. Akasema: Hao wapo nyuma yangu wananifuatia. Na
nimefanya haraka kukujia, Mola wangu Mlezi, ili uridhike.
85. (Mwenyezi Mungu) akasema: Sisi tumewatia mtihani watu
wako baada yako, na Msamaria amewapoteza.
86. Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu
Mlezi hakukuahidini ahadi nzuri? Je, umekuwa muda mrefu kwenu au mmetaka
ikushukieni ghadhabu ya Mola wenu Mlezi, ndio maana mkavunja miadi yangu?
87. Wakasema:
Sisi hatukuvunja miadi yako kwa khiari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya
mapambo ya watu, basi tukaitupa. Na hivyo ndivyo alivyo toa shauri Msamaria.
88. Na
akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti. Na wakasema: Huyu ndiye mungu wenu,
na mungu wa Musa, lakini alisahau.
89. Je!
Hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala hakuweza kuwadhuru wala kuwafaa?
90. Na hakika
Harun alikwisha waambia kabla yake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa
mtihanini tu kwa kitu hiki. Na kwa yakini Mola wenu Mlezi ni Arrahmani, Mwingi
wa Rehema. Basi nifuateni mimi, na t'iini amri yangu!
91. Wakasema: Hatutaacha kumuabudu mpaka Musa atapo rejea
kwetu.
92. (Musa) akasema: Ewe Harun! Ni nini kilicho kuzuia,
ulipo waona wamepotea,
93. Hata usinifuate? Je, umeasi amri yangu?
94. Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu
zangu, wala kichwa changu. Kwa hakika naliogopa usije sema: Umewafarikisha Wana
wa Israil, na hukungojea kauli yangu.
95. (Musa) akasema: Ewe Msamaria! Unataka nini ?
96. Akasema: Niliona wasiyo yaona wao, nikashika gao katika
unyao wa Mtume. Kisha nikalitupa. Na hivi ndivyo ilivyo nielekeza nafsi yangu.
97. (Musa) akasema: Basi ondoka! Na kwa yakini utakuwa
katika maisha ukisema: Usiniguse. Na hakika una ahadi kwako isiyo vunjwa. Na
mtazame huyo mungu wako uliye endelea kumuabudu - Sisi kwa hakika tutamchoma
moto, kisha tutamtawanya baharini atawanyike.
98. Hakika Mungu wenu ni Allah, Mwenyezi Mungu, tu. Hapana
Mungu isipo kuwa Yeye. Ujuzi wake umeenea kila kitu.
99. Namna hivi tunakuhadithia katika khabari za yaliyo
tangulia. Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha ya kukumbukwa.
100. Atakaye jitenga nayo, basi kwa yakini Siku ya Kiyama
atabeba mzigo.
|