21. SURATUL ANBIYAA
(Imeteremka
Makka)
HII NI SURA iliyo teremka Makka
baada ya Surat Ibrahim. Aya
zake ni 112. Inabainisha kukaribia Kiyama na hali washirikina wameghafilika
nacho. Nao walidai kuwa Mtume hatokuwa binaadamu, na pengine wakisema kuwa hii
Qur'ani ni uchawi, na pengine kuwa ni mashairi, na pengine ni ndoto za ovyo
ovyo. Na maonyo yapo mbele yao. Na Mitume wote hawakuwa ila ni wanaadamu tu
kama Muhammad s.a.w., na walio watangulia kabla yao walisema uwongo kama
walivyo sema uwongo Makureshi. Mwenyezi Mungu aliwajaalia ajali yao, kwani Yeye
ni Mweza wa kuteketeza na kubakisha, na ni vyake Yeye vyote viliomo katika
mbingu na ardhi. Na Malaika kila walipo wanamtakasa kwa kumsabihi Mwenyezi
Mungu Mtukufu wala hawasiti. Na hakika kwenda sawa mbingu na ardhi ni dalili
kuwa Muumba wake ni Mmoja, kwani lau kuwa wangeli shirikiana waumbaji mambo
yangeli fisidika. Na Mitume wote wamekuja na amri ya kuabudiwa Mwenyezi Mungu
peke yake. Wala hana mwana, wala asiseme yeyote kuwa yeye ni mungu pamoja na
Mwenyezi Mungu. Wasemao hivyo malipo yao ni Jahannamu. Na Subhanahu kabainisha
utukufu wa viumbe vyake, na ajabu za uumbaji wake wa mbingu na ardhi. Na
akabainisha hali ya washirikina na makafiri. Naye Subhanahu wa Taa'la
amenabihisha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo wahifadhi watu, na akaashiria
Subhanahu nini malipo ya makafiri Siku ya Kiyama. Na akataja hadithi ya Musa na
Harun pamoja na Firauni, na hadithi ya Ibrahim pamoja na kaumu yake, na alivyo
mneemesha kwa dhuriya wema. Naye Subhanahu wa Taa'la ametaja hadithi ya Luut'
na kaumu yake, na walivyo angamizwa, na hadithi ya Nuhu a.s. na ukafiri wa
kaumu yake, na walivyo teketezwa isipo kuwa walio amini. Kisha Subhanahu wa
Taa'la akaashiria hadithi za Sulaiman, na Daud, na Ayub, na Ismail, na Idris,
na Dhulkifli, na Dhunnuun, na Maryamu. Na akataja khabari za Juj na Maajuj.
Naye Subhanahu amebainisha vitendo vyema na matunda yake, na malipo watayo
lipwa wenye kumchamngu na wakatenda mema, na hali yao Siku ya Kiyama, na rehema
ya Mwenyezi Mungu katika Ujumbe wa Muhammad, na maonyo ya Mwenyezi Mungu kwa
washirikina. Na kwamba hakika amri yote ni yake Yeye anavyo hukumu, na Yeye
ndiye Mbora wa mahakimu.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|