24. SURATUN NUR
(Imeteremka
Madina)
Sura hii ni ya Madina, na
Aya zake ni 64. Mwenyezi Mungu amebainisha ndani yake waajibu wa kusafisha umma
na uchafu wa zina na kutangaza fedheha kwa vitendo na maneno kati ya Waumini.
Na akaleta sharia ya adhabu kuzuia hayo, kama alivyo leta sharia makhsusi
katika uzinzi wa mume au mke ili kujenga imani baina ya mtu na mkewe. Kutoka
uzinzi masimulizi yakaingilia kutaja hukumu ya uwongo katika hali hizi, na
yawapasayo Waumini kwa min tarafu ya neno ovu lisio kuwa na dalili. Tena
yakafuatia masimulizi ya adabu za kuingia majumbani. Na nani mwenye haki
ya kuona pambo la mwanamke. Na baada ya wito wa jumla ikafuatiliza kutakiwa
mwendo safi usio na towa. Kisha imekuja Nuru ya Mwenyezi Mungu, na inatajwa
misikiti, na vinatangazwa vitendo vya makafiri na hali za wenye inadi. Na
upande mwengine zinaelezwa hali za Waumini. Baada ya hayo Sura inaeleza adabu
za watu wa nyumbani, watu walio khusiana, watoto na wakubwa, katika hali ya
kuingiliana na kuchanganyika. Na nani mwenye haki ya kula naye mtu. Na
khatimaye zimetajwa sifa za Waumini wanapo itwa na Mtume kwa jambo lilio
wakhusu wote, na Sura ikambainisha Mwenye Ukuu wa Ufalme wake ulio tukuka, na Mwenye
kuenea ujuzi wake.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|