1 - 50
1. HII NI SURA Tuliyo iteremsha na tukailazimisha;
tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.
2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila
mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika
hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini.
3. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke
mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina.
Na hayo yameharimishwa kwa Waumini.
4. Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete
mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao
tena. Na hao ndio wapotovu.
5. Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na
wakatengenea; kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
6. Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila
nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo
cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
7. Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu
yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.
8. Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne
kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyu mume ni miongoni mwa waongo.
9. Na mara ya tano ya kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe
juu yake kama mumewe yu miongoni mwa wanao sema kweli.
10. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na
rehema yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba....
11. Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu.
Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata
aliyo yachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni
mwao, atapata adhabu kubwa.
12. Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na
wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
13. Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa
hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo.
14. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na
rehema yake katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa
kwa sababu ya yale mliyo jiingiza.
15. Mlipo yapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa
vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni
kubwa.
16. Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii
kuzungumza haya. Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!
17. Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama
haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!
18. Na Mwenyezi Mungu anakubainisheni Aya. Na Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
19. Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio
amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua
na nyinyi hamjui.
20. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na
rehema yake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu....
21. Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na
atakaye fuata nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau
kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika
miongoni mwenu kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
22. Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape
kutowapa jamaa zao na masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie mbali. Je!
Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.
23. Hakika wanao
wasingizia wanawake, wanao jihishimu, walio ghafilika, Waumini, wamelaaniwa duniani
na Akhera, nao watapata adhabu kubwa.
24. Siku ambayo
zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyo kuwa
wakiyatenda.
25. Siku hiyo
Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kwamba hakika
Mwenyezi Mungu ndiye Haki Iliyo Wazi.
26. Wanawake
waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na wanawake
wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao wameepushwa
na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.
27. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu
mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate
kukumbuka.
28. Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe.
Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu
anajua mnayo yatenda.
29. Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisio kaliwa ambazo
ndani yake yamo manufaa yenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yadhihirisha na
mnayo yaficha.
30. Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na
wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari
za wanayo yafanya.
31. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na
wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na
waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa
waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume
zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao,
au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio,
au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao
ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu,
enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.
32. Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa
wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa
fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.
33. Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea,
mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa
uhuru katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama
mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala
msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la
maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi
Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
34. Na kwa yakini tumekuteremshieni Ishara zilizo wazi na
mifano kutokana na walio tangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu.
35. Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa
Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota
inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa,
mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake
kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu
humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
36. Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha
zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni
37. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na
kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku
ambayo nyoyo na macho yatageuka.
38. Ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo yatenda, na
awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya
hisabu.
39. Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi)
uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na
atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwepesi wa kuhisabu.
40. Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na
mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu
mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na
nuru hawi na nuru.
41. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo
katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua
Sala yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua
wayatendayo.
42. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na
kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya wote.
43. Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu,
kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati
yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu
nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake
kupofua macho.
44. Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika
katika hayo yapo mazingatio kwa wenye kuona.
45. Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na
maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu
miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
46. Kwa yakini tumeteremsha Ishara zinazo bainisha. Na
Mwenyezi Mungu hummwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
47. Na wanasema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na
tumet'ii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye
kuamini.
48. Na wanapo itwa kumuendea Mwenyezi Mungu na Mtume wake
ili ahukumu baina yao, kipo kikundi katika wao kinakataa.
49. Na ikiwa haki ni yao, wanamjia kwa kut'ii.
50. Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wanaona shaka, au
wanaogopa ya kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali hao ndio
madhaalimu.
|