25. SURAT AL FURQAN
(Imeteremka
Makka)
Idadi ya Aya za Sura hii ni
77. Zote ni za Makka isipo kuwa Aya 68, 69 na 70.
Sura imeanzia kwa kubainisha cheo cha Qur'ani, na ukubwa wa ufalme wa Mwenye
kuiteremsha ambaye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na juu ya utukufu wa
utawala wake, washirikina bado badala yake wanaabudu masanamu, na
wanaikadhibisha Qur'ani, na wanaukataa Utume wa Mtume s.a.w. kwa hoja ya kuwa
ati yeye ni binaadamu, anakula chakula, na anatembea masokoni, na kwa ubishi
wanataka Malaika ndio wawaletee Ujumbe. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amewafanya
Mitume wake Malaika angeli wafanya ni watu ili wapate kufahamiana na watu.
Ubabaishi unge baki. Na wakapinga kwa nini Qur'ani ikawa inateremka vipande
vipande. Wakajibiwa hikima ya hayo. Na inda hii ikafuatilizwa kwa mifano yenye
kueleza khabari za Mitume waliyo pita na kaumu zao. Lakini hizo kaumu zikafuata
matamanio yao. Wakawa kama wanyama au wapotovu zaidi katika mwendo wao. Na
zikaja Aya za uumbaji zenye kuonyesha ukamilifu wa kudra yake Mtukufu, yenye
kufahamisha uangalizi na maarifa. Na Sura ikakhitimisha kwa kutaja sifa za
Waumini zitazo warithisha vyumba vya Peponi vya juu, watapo pokewa kwa maamkio
na kusalimiwa.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|