1 - 50
1. Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe
mwonyaji kwa walimwengu wote.
2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na
mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na
akakikadiria kwa kipimo.
3. Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote,
bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki
mauti, wala uhai, wala kufufuka.
4. Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi
alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma
na uwongo.
5. Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo
viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni.
6. Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na
ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
7. Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na
anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?
8. Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani
ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa.
9. Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea,
wala hawataiweza Njia.
10. Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko
hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya
fakhari.
11. Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi
tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa..
12. Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia
hasira yake na mngurumo wake.
13. Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa,
wataomba wafe.
14. Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi!
15. Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo
wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo?
16. Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi
juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa.
17. Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na
akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea
njia?
18. Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu!
Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha
wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia.
19. Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo
hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu
tutamwonjesha adhabu kubwa.
20. Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika
na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi
yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye
kuona.
21. NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi
hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona
bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno!
22. Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo
kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali!
23. Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao,
tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika.
24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora
na mahali penye starehe nzuri.
25. Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na
wateremshwe Malaika kwa wingi,
26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa
Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.
27. Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake,
na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume!
28. Ee Ole
wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!
29.
Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet'ani ni
khaini kwa mwanaadamu.
30. Na
Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii
Qur'ani ni kihame.
31. Na
vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi
anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.
32. Na
wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur'ani kwa jumla moja? Hayo ni
hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.
33. Wala
hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na
tafsiri iliyo bora.
34. Wale
ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao
watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia.
35. Na
hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa
waziri.
36.
Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi
tukawateketeza kabisa.
37. Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume,
tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye
kudhulumu adhabu chungu.
38. Na tuliwaangamiza kina A'di na Thamudi na watu wa Rass
na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao.
39. Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza
kabisa kabisa.
40. Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa
mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa
wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa.
41. Na wanapo
kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi
Mungu aliye mtuma kuwa Mtume?
42. Kwa hakika
alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo
kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea
njia.
43. Je! Umemwona
aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni
wakili wake?
44. Au wewe
unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama
nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.
45. Je! Huoni
jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya
kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake.
46. Kisha
tunakivutia kwetu kidogo kidogo.
47. Naye ndiye aliye
kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni
mchana ni kufufuka.
48. Naye ndiye
anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha
kutoka mbinguni maji safi.
49. Ili kwa hayo
tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba.
50. Na kwa
yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila
kukufuru.
|