51 - 100
51. Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe
makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini.
52. Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu
wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.
53. Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo.
54. (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.
55. Nao wanatuudhi.
56. Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.
57. Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem,
58. Na makhazina, na vyeo vya hishima,
59. Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.
60. Basi wakawafuata lilipo chomoza jua.
61. Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa
wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!
62. (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu
Mlezi. Yeye ataniongoa!
63.
Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana,
na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.
64. Na
tukawajongeza hapo wale wengine.
65. Tukawaokoa
Musa na walio kuwa pamoja naye wote.
66. Kisha
tukawazamisha hao wengine.
67. Hakika
bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini.
68. Na kwa
hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
69. Na
wasomee khabari za Ibrahim.
70. Alipo
mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?
71.
Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.
72. Akasema: Je!
Yanakusikieni mnapo yaita?
73. Au yanakufaeni,
au yanakudhuruni?
74. Wakasema:
Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.
75. Je! Mmewaona
hawa mnao waabudu-
76. Nyinyi na
baba zenu wa zamani?
77. Kwani hakika
hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
78. Ambaye ndiye
aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa,
79. Na ambaye
ndiye ananilisha na kuninywesha.
80. Na ninapo
ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.
81. Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.
82. Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu
Siku ya Malipo.
83, Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na
watendao mema.
84. Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja
baadaye.
85. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.
86. Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni
mwa wapotovu.
87. Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.
88. Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.
89. Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.
90. Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.
91. Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.
92. Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu
93. Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au
wanajisaidia wenyewe?
94. Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu,
95. Na majeshi ya Ibilisi yote.
96. Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:
97.
Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,
98. Tulipo
kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
99. Na
hawakutupoteza ila wale wakosefu.
100. Basi hatuna waombezi.
|