29. SURAT AL A'NKABUT
(Imeteremka
Makka)
SURA HII NI ya Makka, na
idadi ya Aya zake ni 69. Lakini Aya 1 mpaka 11 ziliteremka Madina. Sura
hii imeanzia kwa kubainisha kwamba hapana budi ila Imani ya Waumini itiwe
mitihanini kwa misukosuko na jihadi kwa ajili ya kulinda dola ya Haki na Imani.
Na binaadamu ameusiwa kwa wazazi wake pamoja na amri ya jihadi, ili ukusanyike
wema na jihadi, na baina ya watu wa namna mbali mbali na Imani. Na imeelezwa
kwamba miongoni mwao yupo anaye sema kwa ulimi wake kwamba ameamini na hali
moyo wake haukukubali. Kisha Sura hii imetaja khabari za Nuhu na kaumu yake, na
kadhaalika imeeleza kisa cha Ibrahim katika wito wake. Na ikabainisha mafunzo
hayo kwa ajili ya Mtume s.a.w. Kisha ikasimulia jawabu ya watu wa Ibrahim. Na
ikaeleza khabari za Lut'i na kisa cha kaumu yake, na kuteremka kwa Wajumbe
Malaika wa Mwenyezi Mungu kuja kuwahiliki, na wakaokoka ahali zake isipo kuwa
mkewe. Kisha Subhanahu akaashiria kisa cha Shuaibu pamoja na Madyana, na cha
Hud na A'di, na Saleh na Thamud, na kudanganyikiwa kwa Qaruni na Firauni na
Hamani na matokeo ya mwisho wao. Na Yeye Subhanahu amebainisha kwamba kuabudu
masanamu kwa washirikina kunategemea hoja iliyo kuwa dhaifu kabisa kuliko jumba
la buibui. Na kwamba mifano kama hii hawaielewi ila wale wanao tumia akili zao.
Na baada ya hayo Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii wake asijadiliane na Watu wa
Kitabu ila kwa njia nzuri. Na Yeye Subhanahu akaashiria kwamba Nabii s.a.w.
hajui kusoma wala kuandika, na hayo yanazidi kuonyesha Utume wake. Na pia
Subhanahu ametaja ukaidi wa washirikina katika kutaka kwao waletewe miujiza ya
kuiona, nayo wataikataa kama walivyo ikataa kaumu ya Musa na wengineo. Na
akagusia kule kuhimiza kwao kuteremshiwa adhabu. Naye amewabainishia adhabu
itakayo wapata. Naye Subhanahu akataja malipo ya Waumini na Makafiri Siku ya
Kiyama, na akataka watu watazame baada ya hayo ulimwengu na neema za Mwenyezi
Mungu Mtukufu ziliomo ndani yake. Kisha akataja thamani ya uhai wa duniani
ukilinganisha na wa Akhera, na hali ya washirikina katika unyonge wao na
kumkimbilia kwao Mwenyezi Mungu wanapo kuwa katika khofu, na wanapo kuwa na
nguvu na wakawa katika usalama wanavyo mshirikisha Mwenyezi Mungu. Kisha
akaeleza neema zake anazo wapa katika Nyumba Takatifu ya Makka, na wanavyo
zikanya neema hizo. Kisha Mwenyezi Mungu akabainisha fadhila za wanao pigana
Jihadi.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|