1 - 50
1. Alif
Lam Mim (A.L.M.)
2. Je! Wanadhani
watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?
3. Hakika
tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha
walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo.
4. Au
wanadhani wanao tenda maovu kwamba watatushinda? Hukumu mbaya hiyo wanayo
hukumu.
5. Mwenye
kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu
itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
6. Na
anaye fanya juhudi basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake.
Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu.
7. Na
walio amini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na tutawalipa
bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
8. Na
tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia
unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi
ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
9. Na walio amini na wakatenda mema, bila ya shaka
tutawatia miongoni mwa watu wema.
10. Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi
Mungu. Lakini wanapo pewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya
mateso ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka
kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi
Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu?
11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio
amini, na atawatambulisha wanaafiki.
12. Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia
yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao
chochote kile. Hakika hao ni waongo.
13. Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine
pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo
kuwa wakiyazua.
14. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao
miaka elfu kasoro miaka khamsini. Basi tufani liliwachukua, nao ni madhaalimu.
15. Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na
tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote.
16. Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni
Mwenyezi Mungu, na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua.
17. Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi
Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu
hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu
Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa.
18. Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla
yenu zilikwisha kadhibisha. Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi.
19. Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha
uumbaji, na kisha akarudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
20. Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo
anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
21. Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake
Yeye mtapelekwa.
22. Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika
mbingu. Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
23. Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana
naye, hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata
adhabu chungu.
24. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni
au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo
Ishara kwa watu wanao amini.
25. Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya
Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku
ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na
makaazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni.
26. Lut'i akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola
wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
27. Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na
tukajaalia katika dhuriya zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika
dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema.
28. Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi
mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa
hayo.
29. Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na
katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo
kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao
kweli.
30. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu
mafisadi hawa!
31. Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara,
walisema: Hakika sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu
wake hakika wamekuwa madhaalimu.
32. Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi
tunajua zaidi nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo
kuwa mkewe aliye miongoni mwa watao kaa nyuma.
33. Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa
ajili yao, na moyo uliona dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala
usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni
mwa watao kaa nyuma.
34. Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu
kutoka mbinguni kwa sababu ya uchafu wanao ufanya.
35. Na tumeacha katika mji huo Ishara ilio wazi kwa watu wanao
tumia akili zao.
36. Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye
akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera,
wala msende katika ardhi mkifisidi.
37. Lakini walimkanusha basi ukawatwaa mtikiso wa ardhi,
wakapambazukiwa ndani ya nyumba zao nao wamefudikia.
38. Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha
kubainikieni kutokana na maskani zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na
akawazuilia Njia, na hali walikuwa wenye kuona.
39. Na pia Qaruni na Firauni na Hamana! Na Musa aliwajia
kwa Ishara waziwazi, lakini walijivuna katika nchi, wala hawakuweza kushinda.
40. Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake.
Kati yao wapo tulio wapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walio
nyakuliwa na ukelele; na kati yao wapo ambao tulio wadidimiza katika ardhi; na
kati yao wapo tulio wazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu,
lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao.
41. Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi
Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno
kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.
42. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanacho
kiomba badala yake Yeye. Na Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.
43. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu ila
wenye ilimu.
44. Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Kwa
hakika katika hayo ipo Ishara kwa Waumini.
45. SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala.
Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi
Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda.
46. Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri
kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini
yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu
ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.
47. Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani).
Basi wale tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa
hawa (washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa
makafiri.
48. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala
hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka
wavunjifu.
49. Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua
vya walio pewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu.
50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa
Mola wake Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni
mwonyaji mwenye kubainisha tu.
|