1 - 50
1. Alif
Lam Mim.
2. Hiki ni
Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu,
3. Ambao
huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa katika tuliyo wapa.
4. Na
ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na
Akhera wana yakini nayo.
5. Hao
wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio walio fanikiwa.
6. Hakika
wale walio kufuru ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawaamini.
7.
Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao, na juu ya
macho yao pana kifuniko. Basi watapata adhabu kubwa.
8. Na katika watu, wako wasemao: Tumemwamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho, wala wao si wenye kuamini.
9. Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio
amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui.
10. Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu
amewazidishia maradhi. Basi watakuwa na adhabu chungu kwa sababu ya kusema kwao
uwongo.
11. Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni.
Husema: Bali sisi ni watengenezaji.
12. Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui.
13. Na wanapo ambiwa: Aminini kama walivyo amini watu.
Husema: Tuamini kama walivyo amini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini
hawajui tu.
14. Na wanapo kutana na walio amini husema: Tumeamini. Na
wanapo kuwa peke yao na mashet'ani wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi.
Hakika sisi tunawadhihaki tu.
15. Mwenyezi Mungu atawadhihaki wao na atawawacha katika
upotofu wao wakitangatanga ovyo.
16. Hao ndio walio nunua upotofu kwa uwongofu; lakini
biashara yao haikupata tija, wala hawakuwa wenye kuongoka.
17. Mfano wao ni kama mfano wa aliye koka moto, na ulipo
tanda mwangaza wake kote kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawawacha
katika giza, hawaoni.
18. Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea.
19. Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na
radi na umeme; wakawa wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya
mingurumo, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.
20. Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea
mwangaza huenda, na unapo wafanyia giza husimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu
angeliondoa kusikia kwao na kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila
kitu.
21. Enyi
watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu,
ili mpate kuokoka.
22.
(Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu
kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe
riziki zenu. Basi msimfanyizie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua.
23. Na
ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya
mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema
kweli.
24. Na
mkitofanya - na wala hamtofanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni
watu na mawe walio andaliwa hao wanao kanusha.
25. Na
wabashirie walio amini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo
mito kati yake; kila watapo pewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo
pewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyo fanana; na humo watakuwa na wake walio
takasika; na wao humo watadumu.
26. Hakika
Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama
wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi,
lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano
huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila
wale wapotovu,
27. Wanao
vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyo
amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio
wenye khasara.
28. Vipi
mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu akakufufueni! Kisha
atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?.
29. Yeye
ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi. Tena akazielekea mbingu, na
akazifanya mbingu saba. Naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.
30. Na
pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa
(mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga
damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako?
Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua.
31. Na
akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na
akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli.
32.
Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza
Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima.
33.
Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipo waambia majina yake alisema:
Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua
mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha?
34. Na
tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis,
alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri.
35. Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani,
na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa
katika wale walio dhulumu.
36. Lakini Shet'ani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa
katika waliyo kuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi.
Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda.
37. Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola
wake Mlezi alimkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na
Mwenye kurehemu.
38. Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni uwongofu
utokao kwangu, basi watakao fuata uwongofu wangu huo haitakuwa khofu juu yao
wala hawatahuzunika.
39. Na wenye kukufuru na kuzikanusha ishara zetu, hao ndio
watakao kuwa watu wa Motoni, humo watadumu.
40. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo
kuneemesheni, na timizeni ahadi yangu, na Mimi nitatimiza ahadi yenu, na
niogopeni Mimi tu.
41. Na aminini niliyo yateremsha ambayo yanasadikisha mliyo
nayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze Ishara zangu kwa thamani
ndogo. Na niogopeni Mimi tu.
42. Wala msichanganye kweli na uwongo na mkaificha kweli
nanyi mnajua.
43. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na
wanao inama.
44. Je! Mnawaamrisha watu mema na mnajisahau nafsi zenu, na
hali nyinyi mnasoma Kitabu? Basi je,
hamzingatii?
45. Na tafuteni
msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa
kwa wanyenyekevu,
46. Ambao wana
yakini kuwa hakika watakutana na Mola wao Mlezi na ya kuwa hakika watarejea
kwake.
47. Enyi Wana wa
Israili! Kumbukeni zile neema zangu nilizo kuneemesheni, na nikakuteuweni
kuliko wote wengineo.
48. Na iogopeni
Siku ambayo mtu hatomfaa mtu kwa lolote, wala hayatakubaliwa kwake maombezi,
wala hakitapokewa kikomboleo kwake; wala hawatanusuriwa.
49. Na vile
tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya, wakiwachinja
wana wenu wa kiume na wakawawacha hai wanawake; na katika hayo ulikuwa ni
mtihani mkubwa ulio toka kwa Mola wenu Mlezi.
50. Na tulipo
ipasua bahari kwa ajili yenu na tukakuokoeni, tukawazamisha watu wa Firauni, na
huku mnatazama.
|