51 - 69
51. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia
Kitabu hiki wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu
wanao amini.
52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina
yangu na nyinyi. Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini
upotovu na wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri.
53. Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa
hapana wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea
kwa ghafla, na hali wao hawana khabari.
54. Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali
Jahannamu kwa hakika imewazunguka makafiri!
55. Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini
ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda!
56. Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina
wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu.
57. Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu.
58. Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka
tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu
humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao,
59. Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
60. Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao!
Mwenyezi Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia
Mwenye kujua.
61. Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na
akafanya jua na mwezi kuti'ii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi
Mungu. Wapi basi wanako geuzwa?
62. Mwenyezi
Mungu humkunjulia, na humdhikishia, riziki amtakaye katika waja wake. Kwa
hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
63. Na
ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi
baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu
Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao
hawafahamu.
64. Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na
mchezo. Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua!
65. Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi
Mungu kwa kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara
wanamshirikisha.
66. Wapate kuyakanya tuliyo wapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja jua!
67. Je!
Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine
wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu, na neema za
Mwenyezi Mungu wanazikataa?
68. Na
nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu au anaye
kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya makafiri?
69. Na
wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika
Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.
|