30. SURAT AR-RUM
(Imeteremka
Makka)
SURA hii imeanza kutaja
kushindwa kwa dola ya Rumi, na ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa Waumini kwamba
atawapa ushindi kuwashinda Waajemi, na ikawataka watu wafikiri juu ya uumbaji
wa Mwenyezi Mungu, na watembee katika ardhi wapate kuujua mwisho wa makafiri
walio iamirisha ardhi zaidi kuliko walivyo iamirisha wao Makureshi. Na Sura hii
imeeleza hali ya watu Siku ya Kiyama, na ikasifu kutakasa kwa Waumini kumtakasa
Mwenyezi Mungu, na wanavyo muabudu Yeye asubuhi mapema na jioni, na adhuhuri na
alasiri. Na ikanabihisha dalili za Upweke wake Mwenyezi Mungu kwa kupishana zamu
usiku na mchana, na kukhitalifiana lugha, na mambo yanayo onekana ya ulimwengu
katika mbingu na ardhi. Na ikapiga mifano ambayo inayo onyesha upotovu wa
shirki, na ikawakumbusha watu vipi Mwenyezi Mungu alivyo waumba wao na
akawaneemesha, na kuvitia nguvu viungo vya ukoo, na kushikamana kwa ujamaa, na
ikashughulikia mambo ya sharia, ikaharimisha riba, na ikalazimisha Zaka, na
ikahimiza kuwafanyia wema jamaa.
Kisha Mwenyezi Mungu Subhanahu akawaneemesha waja wake na akawataka washike
Dini na ut'iifu, na akawataka waangalie katika ulimwengu yale maajabu yake
yanayo onyesha ukomo wa nguvu na uweza. Na akabainisha mabadiliko ya binaadamu
anavyo geuka mpaka akafikia umri wa ukongwe kabisa.
Na Aya za mwisho zimegusia Siku ya Kiyama na jinsi washirikina wanavyo
ikanya. Na Sura ikakhitimishia kwa kumnasihi Mtume s.a.w. athibiti juu ya Haki,
na avumilie kwa yanayo mfika, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu inakuja tu bila ya
muhali wowote.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|