1 - 50
1. Alif
Lam Mim (A.L.M.)
2. Warumi
wameshindwa,
3. Katika
nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda
4. Katika miaka
michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo
Waumini watafurahi.
5. Kwa nusura ya
Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
6. Ni ahadi ya
Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui.
7. Wanajua hali
ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera.
8. Je!
Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo
ndani yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka
ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi.
9. Je!
Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Nao
walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakaitimbua ardhi na wakaistawisha zaidi
kuliko walivyo istawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi.
Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu
nafsi zao.
10. Kisha
ulikuwa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na
wakawa wanazifanyia maskhara.
11. Mwenyezi
Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa
kwake.
12. Na itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa.
13. Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa
wakiwashirikisha na Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao.
14. Na siku itapo simama Saa, siku hiyo watagawanyika.
15. Ama walio amini na wakatenda mema watafurahishwa katika
Bustani.
16. Na ama walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu na
mkutano wa Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu.
17. Basi Subhanallah! Mtakaseni Mwenyezi Mungu jioni na
asubuhi,
18. Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na
alasiri na adhuhuri.
19. Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na
hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa
kwake. Na kama hivyo ndivyo mtavyo fufuliwa.
20. Na katika Ishara zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo.
Kisha mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote.
21. Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu
kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma
baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
22. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na
kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa
wajuzi.
23. Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana,
na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara
kwa watu wanao sikia.
24. Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni
khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua
ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao
zingatia.
25. Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi
zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka
kwenye ardhi.
26. Na vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote
vinamt'ii Yeye.
27. Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha
mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano
bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
28. Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika
hao iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo
kuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyo
ogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye
akili.
29. Bali walio dhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina
kujua. Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao
hawatakuwa na wa kuwanusuru.
30. Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo
umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji
wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi
hawajui.
31. Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni
Sala, na wala msiwe katika washirikina.
32. Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na
wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho.
33. Yakiwapata watu madhara humwomba Mola wao Mlezi nao
wametubu kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni
mwao humshirikisha Mola wao Mlezi,
34. Kwa kuyakataa tuliyo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua!
35. Au tumewateremshia hoja ambayo kwayo ndio wanafanya
ushirikina?
36. Na watu tunapo waonjesha rehema huifurahia, na
ukiwasibu uovu kwa iliyo yatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa.
37. Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki
amtakaye na humdhikisha amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao
amini.
38. Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo
ni kheri kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa.
39. Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya
watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka
kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa.
40. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, kisha
akakuruzukuni, kisha anakufisheni, na kisha anakufufueni. Je! Yupo yeyote
katika hao mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye
ametakasika, na ametukuka na hayo mnayo mshirikisha naye.
41. Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya
mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda
wakarejea kwa kutubu.
42. Sema: Safirini duniani muangalie ulikuwaje mwisho wa
walio tangulia. Wengi wao
walikuwa washirikina.
43. Basi
uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyo
zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana.
44. Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake
mwenyewe, na anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao.
45. Ili awalipe walio amini na wakatenda mema kutokana na
fadhila yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri.
46. Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara
njema, na ili kukuonjesheni baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yende kwa
amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru.
47. Na hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao, na
wakawajia kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale walio fanya ukosefu. Na
ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini.
48. Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma pepo zikayatimua
mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande
mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapo wafikishia awatakao katika
waja wake, mara hao huwa na furaha.
49. Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata
tamaa.
50. Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu,
jinsi anavyo ihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye bila ya
shaka Mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
|