31. SURAT LUQMAN
(Imeteremka
Makka)
Imeanza Sura hii tukufu kwa
kueleza khabari za hichi Kitabu na uwongofu na rehema ziliomo ndani yake. Na
wamesifiwa watu wema kwa kuwa wana ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, na wanaiamini
Akhera, na watapata mafanikio. Na kinyume cha hayo yametajwa ya walio potea,
wenye kiburi. Na wamebashiriwa Waumini kuwa watapata malipo mazuri katika
makaazi ya Peponi. Na macho yanatakiwa yaangalie Ishara za ulimwengu zinazo
onyesha uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Upweke wake. Na Sura hii inawakabili
makafiri kwa kuwaambia kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu wanaye muwekea
washirika ameumba asicho kiweza yeyote asiye kuwa Yeye kukiumba. Tena Sura
ikaingia kutaja wasia wa Luqman kumuusia mwanawe mausio yaliyo changanyika na
mausio ya mtu na wazazi wake. Na ikaeleza mambo aliyo yat'iisha Mwenyezi Mungu
kwa faida ya mwanaadamu, na neema zinazo onekana na zisio onekana alizo mjazia
mwanaadamu.
Na ikaeleza khabari za wanao jadili mambo yaliyo mkhusu Mwenyezi Mungu bila ya
ujuzi, na wanao toa udhuru kwa upotovu wao kuwa wanawafuata waliyo kuwa
wakiyafuata baba zao. Na Sura ikamsifu anaye uelekeza uso wake kwa Mwenyezi
Mungu naye akawa ni mtenda mema, na ikamnasihi Mtume asihuzunike kwa kukataa
kwa mwenye kukufuru, kwani marejeo ya huyo ni kwa Mwenyezi Mungu. Na ikafafanua
kwa wingi mambo yanayo onyesha uweza, na utukufu, na rehema.
Na Sura imeamrisha kumcha Mwenyezi Mungu, na kuogopa hisabu na malipo. Na
imehadharisha ghururi, kudanganyika, na kumt'ii Shet'ani. Na ikakhitimisha kwa
kutaja kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye ujuzi kamili wa kila kitu. Na
muhimu ya iliyo kusanya Sura hii ni mambo matatu:
Kwanza: Kuwabashiria
watu wema kuwa watapata neema na furaha, na kuwaonya makafiri kuwa watapata
adhabu.
Pili: Kueleza Ishara za
ulimwengu na mambo yaliyo wazi yenye kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu, na
Upweke wake, na upeo wa utukufu wake na rehema yake.
Tatu: Wasia mkuu ulio
kusudiwa usalama wa itikadi, na kulinda ut'iifu na tabia njema.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Alif
Lam Mim (A.L.M.)
2. Hizi ni
Aya za Kitabu chenye hikima.
3. Kuwa ni
Uwongofu na Rehema kwa wafanyao wema,
4. Wanao
shika Sala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na Akhera.
5. Hao
ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio wenye kufanikiwa.
6. Na
miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na
njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata
adhabu ya kuwafedhehesha.
7. Na (mtu
kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba
hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata
adhabu chungu.
8. Hakika walio amini na wakatenda mema watakuwa nazo
Bustani za neema.
9. Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na
Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
10. Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka
katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya
wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea
mizuri ya kila namna.
11. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni
wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo
dhaahiri.
12. Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru
Mwenyezi Mungu. Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi
yake. Na aliye kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.
13. Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe
mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka
ni dhulma iliyo kubwa.
14. Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake
ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya
miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.
15. Na pindi
wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat'ii. Lakini
kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anaye elekea kwangu. Kisha
marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
16. Ewe
mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali
au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote.
17. Ewe
mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo
kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa..
18. Wala
usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu
hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha.
19. Na ushike
mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila
ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda.
20. Kwani
hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni viliomo mbinguni na
kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na za siri? Na miongoni
mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo ilimu, wala uwongofu,
wala Kitabu chenye nuru.
21. Na wanapo
ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali tunafuata tuliyo
wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani anawaita kwenye adhabu ya Moto
uwakao?
22. Na mwenye
kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa anafanya wema, basi huyo
hakika amekwisha kamata fundo lilio madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni kwa
Mwenyezi Mungu.
23. Na anaye
kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio yao, na hapo tutawaambia
waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
24.
Tunawastarehesha kwa uchache, kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu.
25. Na
ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi
Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
26. Ni vya
Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu
ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
27. Na lau
kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na
ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli
kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
28.
Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi moja tu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
29. Kwani
huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana
katika usiku, na amedhalilisha jua na mwezi? Vyote hivyo vinakwenda mpaka
wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
30. Hivi
ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na hakika wanacho kiomba ni
cha uwongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mtukufu na ndiye Mkubwa.
31. Kwani
huoni kwamba marikebu hupita baharini zikichukua neema za Mwenyezi Mungu, ili
kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake? Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila
mwenye kusubiri, mwenye kushukuru.
32. Na
wimbi linapo wafunika kama wingu, wao humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia
dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo baadhi yao huenda mwendo wa
sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini kafiri mkubwa.
33. Enyi
watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana,
wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya
kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi
Mungu mdanganyifu.
34. Hakika
kuijua Saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye anaye iteremsha
mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi
yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.
|