32. SURAT ASSAJDAH
(Imeteremka
Makka)
Sura hii iliteremka baada ya Surat Al Muuminun. Nayo imekusanya mazungumzo
juu ya kuteremshwa Kitabu, na umuhimu wa Mtume s.a.w., na kuumbwa mbingu na
ardhi, na shani yake Mtukufu katika kupanga, na kumlea na kumuendeleza kumuumba
mwanaadamu, na maneno ya wenye kukanya kufufuliwa na jawabu ya kuwajibu, na
hali ya wakosefu Siku ya hisabu, na msimamo wa Waumini wakati zinapo tajwa Aya,
na kubainisha malipo ya Waumini na waovu, na kuteremshiwa Musa a.s. Taurati, na
vipi alivyo waamili Mwenyezi Mungu Wana wa Israili, na kuwaelekeza makafiri wa
Makka wazingatie walivyo angamia walio watangulia, na kuwataka watazame kwa
macho yao ili waamini kufufuliwa. Na Sura imetaja vipi hao makafiri walivyo
ifanyia kejeli siku ya ushindi, na jawabu walio pewa.
Na lengo muhimu la Sura hii ni kuelekeza nadhari kwenye Ishara za
ulimwengu ulivyo umbwa, na mazungumzo juu ya kufufuliwa, na jawabu za kuwarudi hao
wanao kanya kufufuliwa, na kuwaelekeza makafiri wazingatie maangamizo yaliyo
wasibu walio watangulia.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Alif
Lam Mim (A.L.M.)
2. Huu ni
mteremsho wa Kitabu kisicho kuwa na shaka yoyote kinacho toka kwa Mola Mlezi wa
walimwengu wote.
3. Au wanasema:
Amekizua? Bali hichi ni Kweli iliyo toka kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu
wasio fikiwa na mwonyaji kabla yako; huenda wakaongoka.
4. Mwenyezi
Mungu ndiye aliye umba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa siku sita, na
akatawala kwenye Kiti cha Enzi. Nyinyi hamna mlinzi wala mwombezi isipo kuwa
Yeye tu. Basi, je, hamkumbuki?
5. Anapitisha
mambo yote yalio baina mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku ambayo
kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyo hisabu nyinyi.
6. Huyu ndiye
Mwenye kuyajua yasiyo onekana na yanayo onekana. Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
7. Ambaye ametengeneza
vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo.
8. Na kisha
akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu.
9. Kisha
akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona, na
nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru.
10. Nao husema:
Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya?
Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi.
11. Sema:
Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa
Mola wenu Mlezi.
12. Na ungeli
waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema):
Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia. Turejeshe tukatende
mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa.
13. Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake.
Lakini imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu : Kwa yakini nitaijaza Jahannamu
kwa wote hawa, majini na watu.
14. Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu
hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo
kuwa mkiyatenda.
15. Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao
wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa
kumhimidi, nao hawajivuni.
16. Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao
Mlezi kwa khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku.
17. Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo
furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda.
18. Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi sawa.
19. Ama
walio amini na wakatenda mema, watakuwa nazo Bustani za makaazi mazuri. Ndio pa
kufikia kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
20. Na ama wale walio tenda uovu, basi makaazi yao ni
Motoni. Kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni
adhabu ya Moto ambayo mliyo kuwa mkiikanusha.
21. Na tutawaonjesha adhabu khafifu kabla ya adhabu kubwa,
huenda labda watarejea.
22. Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye kumbushwa
kwa Ishara za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi tutajilipiza kwa
wakosefu.
23. Hakika Sisi tulikwisha mpa Musa Kitabu. Basi usiwe na
shaka kuwa kakipokea. Na tukakifanya kuwa ni uwongofu kwa Wana wa Israili.
24. Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu
kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu.
25. Hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye fafanua baina yao
Siku ya Kiyama katika waliyo kuwa wakikhitalifiana.
26. Je! Haijawabainikia kwamba kaumu ngapi tuliziangamiza
kabla yao, nao wanapita katika maskani zao hizo? Hakika katika hayo zipo Ishara. Basi, je,
hawasikii?
27. Je! Hawaoni ya
kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayo
kula wanyama wao na wao wenyewe? Je! Hawaoni?
28. Wanasema:
Ushindi huu ni lini, kama mnasema kweli?
29. Sema: Siku
ya Ushindi, wale walio kufuru imani yao haitawafaa kitu, wala wao hawatapewa
muhula.
30. Basi
wapuuze, nawe ngonja; hakika wao wanangoja.
|