1 - 50
1. Ewe
Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
2. Na fuata
uliyo funuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu
anazo khabari ya mnayo yatenda.
3. Na
mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.
4.
Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake.
Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya
mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni
wana wenu khasa. Hayo ni
maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye
anaye ongoa Njia.
5. Waiteni kwa
baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa
hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si
lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya
nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
6. Nabii ni bora
zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na jamaa ni
karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini wengine na
Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Haya yamekwisha andikwa
Kitabuni.
7. Na tulipo
chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa
Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu,
8. Ili (Mwenyezi
Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri
adhabu chungu.
9. Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu
zilio juu yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na
majeshi msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
10. Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu;
na macho yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi
Mungu dhana mbali mbali.
11. Hapo ndipo Waumini walipo jaribiwa, na wakatikiswa
mtikiso mkali.
12. Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika
nyoyo zao: Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu.
13. Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi
watu wa Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao
likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa
tupu; hawakutaka ila kukimbia tu.
14. Na lau kuwa wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha
wakatakiwa kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu.
15. Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake
kwamba hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.
16. Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti
au kuuwawa, na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu.
17. Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi
akikutakieni uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi
isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na
wanao waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.
19. Wana
choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka,
kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka
wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao
hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha vitendo vyao. Na hayo kwa
Mwenyezi Mungu ni mepesi.
20.
Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi
watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza khabari zenu.
Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu.
21. Hakika
nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji
Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.
22. Na
Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu
na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo
hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu.
23. Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo
ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea,
wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.
24. Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli
wao, na awaadhibu wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
25. Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya
ghadhabu yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini
katika vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza.
26. Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika
Watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao.
Baadhi yao mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka.
27. Na akakurithisheni ardhi zao na nyumba zao na mali zao,
na ardhi msiyo pata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila
kitu.
28. Ewe
Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi
njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri.
29. Na
ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi
Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa.
30. Enyi
wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu, atazidishiwa
adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
31. NA
MIONGONI mwenu atakeye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema,
tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu.
32. Enyi
wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha
Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo
wake. Na semeni maneno mema.
33. Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa
majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni
uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara.
34. Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za
Mwenyezi Mungu na hikima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri,
na Mwenye khabari.
35. Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na
Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake,
na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na
wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na
wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na
wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake,
Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.
36. Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa
na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika
jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea
upotofu ulio wazi.
37. Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha,
nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha
nafsini mwako aliyo taka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali
Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja
naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa
kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya
Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa.
38. Hapana ubaya kwa Nabii kufanya aliyo mhalalishia
Mwenyezi Mungu. Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa walio pita zamani. Na
amri ya Mwenyezi Mungu ni kudura iliyo kwisha kadiriwa.
39. (Hao wa zamani) walio kuwa wakifikisha risala za Mwenyezi
Mungu na wanamwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhisabu.
40. Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni
Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa
kila kitu.
41. Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa
kumdhukuru. .
42. Na mtakaseni asubuhi na jioni.
43. Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni
gizani mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.
44. Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: Salama!
Na amewaandalia malipo ya ukarimu.
45. Ewe
Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na mwonyaji,
46. Na
mwitaji kumwendea Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa yenye kutoa nuru.
47. Na
wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayo toka kwa Mwenyezi Mungu.
48. Wala
usiwat'ii makafiri na wanaafiki, na usijali udhia wao. Nawe mtegemee Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.
49. Enyi mlio amini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha
mkawapa t'alaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayo ihisabu. Basi
wapeni cha kuwaliwaza, na muwawache kwa kuwachana kwa wema.
50. Ewe Nabii!
Tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na ulio wamiliki kwa mkono
wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu, na mabinti ami zako, na mabinti
wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama yako
walio hama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama
mwenyewe Nabii akitaka kumwoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine.
Sisi tunajua tuliyo wafaridhia wao katika wake zao na wanawake ilio wamiliki
mikono yao ya kulia. Ili isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
|