35. SURAT FAAT'IR
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imefunguliwa kwa
kumsifu Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi, bila ya ruwaza, Mwenye
kuwafanya Malaika kuwa ni wajumbe wa kuwatuma kwa waja wake. Malaika hao wana
mbawa za idadi namna mbali mbali. Fadhila yoyote anayo wapelekea watu hapana wa
kuizuia; na anayo izuia hapana wa kuipeleka. Mwenyezi Mungu anawataka watu
waikumbuke neema, kwani hapana muumba mwengine aliye pamoja naye wa kuwapa
riziki, wala hapana mungu pamoja naye wa wao kumwendea. Na watu wamekanusha
wito wako. Lakini wewe unayo mazingatio kwa yaliyo wapitia Mitume walio
tangulia. Nawe unayo ya kukuliwaza kwa tulivyo ahidi kuwa watarejea kwetu. Na
waajibu kwa watu wasidanganyike na dunia na mapambo yake. Na asiwadanganye
Shet'ani. Na shauri yake ni fupi, haipindukii kuliko kuwapelekea hao wafwasi
wake kwenye maangamizo. Na mwenye kumfuata atamwongoza ampeleke Motoni. Wala
hawawi sawa, mwenye kumpambia Shet'ani vitendo vyake viovu, na aliye muacha.
Ilivyo kuwa shani ya watu ni hiyo, basi usisikitike kwa kuto amini kwao. Kwani
Mwenye kuyapeleka mawingu na akahuisha kwayo kilicho kufa, atawafufua wafu kwa
ajili ya hisabu na malipo. Mwenye kutaka nguvu atafute nguvu kwa Mwenyezi
Mungu. Na mwenye kutafuta nguvu kwa mwenginewe, atamdhalilisha. Na vitendo vya
waja vinapanda kwendea kwake. Yeye, basi huvikubali vitendo vya Waumini,
na huviangusha vitendo vya makafiri. Na dalili ya uweza wake kufufua na
kukusanya Siku ya Kiyama, ni kuwa kamuumba mwanaadamu kutokana na udongo kisha
kutokana na tone la manii, tena akawafanya mwanamume na mwanamke. Wala mwanamke
hachukui mimba wala hazai ila kwa ujuzi wake. Ameumba utamu na chumvi, na
katika vyote hivyo unapata riziki. Na akauingiza usiku katika mchana, na mchana
katika usiku. Na akafanya jua na mwezi yat'ii, kila kimoja wapo kinakwenda kwa
muda maalumu. Muweza huyu ndiye Mungu wa Haki. Na hao wanao waomba badala yake
hawamiliki, na wakiitwa hawasikii, na wakisikia hawajibu. Na Siku ya Kiyama hao
wataukataa ushirikina walio washirikisha na Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni
Muadilifu, anambebesha kila mtu a'mali yake. Na wanaelekezwa Mitume wawakusudie
kwa wito wao wale wanao mwogopa Mwenyezi Mungu. Na kazi ya Mtume ni kuwaonya
watu wake. Na hapana umma wowote ila ulipitiwa na Mwonyaji.
Sura tena inarejea kwenye dalili za uweza, kudra ya Mwenyezi Mungu. Kwa maji
yanatokea mazao ya kila namna, na katika mawe ya majabali yapo namna mmbali
mbali, nyeupe, nyekundu na nyeusi. Na watu na wanyama pia zinakhitalifiana
rangi zao. Yote hayo yanapelekea kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Na mwenye kusoma
kitabu cha Mwenyezi Mungu alicho mrithisha aliye mteuwa ataingia Peponi
astarehe humo. Na mwenye kukufuru ataingia Motoni, hakuna mwisho huko, wala
kupunguziwa adhabu yake. Atataka arejezwe duniani ili atengeneze vitendo vyake,
naye alikwisha pewa muhula wa kukumbuka lau kuwa ni mwenye kukumbuka. Na
aliwajia Mwonyaji. Na Yeye, Subhanahu amekufanyeni ni warithi wa walio tangulia
katika ardhi. Naye anaizuia mbingu isiondoke. Na wenye inadi waliapa kwamba
akiwajia Mwonyaji hapana shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko wlio watangulia.
Alipo wajia wakatakabari, basi vitimbi vyao vikawaangukia wenyewe. Na wao
hawakumkadiria Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kukadiriwa. Na lau kuwa Mwenyezi
Mungu angeli wachukulia watu wa duniani kwa wanayo yafanya asingeli mwacha
mnyama yoyote. Lakini anaakhirisha mpaka muda wao. Ukifika basi hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu
na ardhi, aliye wafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu-
tatu, na nne-nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Muweza juu ya kila kitu.
2. Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana
wa kuizuia. Na anayo izuia hapana wa kuipeleka isipo kuwa Yeye. Naye ndiye
Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
3. Enyi
watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine
asiye kuwa Mwenyezi Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana
mungu ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa?
4. Na wakikukanusha, basi walikwisha kanushwa Mitume kabla
yako. Na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.
5. Enyi
watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha
ya dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Mwenyezi Mungu.
6. Hakika
Shet'ani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi
lake liwe katika watu wa Motoni.
7. Walio
kufuru watakuwa na adhabu kali; na walio amini na wakatenda mema watapata
msamaha na ujira mkubwa.
8. Je!
Yule aliye pambiwa a'mali zake mbaya na akaziona ni njema - basi hakika
Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa amtakaye. Basi nafsi
yako isijihiliki kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anajua wanayo
yafanya.
9. Na
Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma Pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha
kwenye nchi iliyo kufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndivyo kama hivyo
kutakavyo kuwa kufufuliwa.
10. Mwenye
kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye hupanda
neno zuri, na a'mali njema Yeye huitukuza. Na wanao panga vitimbi vya maovu
watapata adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaondokea patupu.
11. Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kisha
kwa tone la manii. Kisha akakufanyeni mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote
hachukui mimba, wala hazai, ila kwa ilimu yake. Na wala hapewi umri mwenye umri
mrefu, wala hapunguziwi katika umri wake, ila yamo hayo katika Kitabu. Hakika
hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.
12. Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye
ladha, mazuri kunywa. Na haya ni ya
chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula nyama mpya (isiyo chacha).
Na mnatoa mapambo mnayo yavaa. Na unaona ndani yake marikebu zinakata maji ili
mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.
13. Anauingiza
usiku katika mchana, na anauingiza mchana katika usiku. Na amelifanya jua na
mwezi kutumikia. Kila kimojapo kinakwenda kwa muda maalumu. Huyo ndiye Mwenyezi
Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnao waomba badala yake
hawamiliki hata ugozi wa kokwa ya tende.
14. Mkiwaomba hawasikii
maombi yenu; na hata wakisikia hawakujibuni. Na Siku ya Kiyama watakataa
ushirikina wenu. Na hapana atakaye kupa khabari vilivyo kama Yeye Mwenye
khabari.
15. Enyi
watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kujitosha, Msifiwa.
16. Akitaka atakuondoeni na alete viumbe vipya.
17. Na hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu.
18. Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Na aliye topewa na
mzigo wake akiomba uchukuliwe hautachukuliwa hata kidogo, na angamwomba jamaa
yake. Hakika wewe unawaonya wale wanao mcha Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na
wanashika Sala. Na anaye jitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na
marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.
19. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani.
20. Wala giza na mwangaza.
21. Wala kivuli na joto.
22. Wala hawalingani walio hai na maiti. Hakika Mwenyezi
Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio
makaburini.
23. Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.
24. Hakika Sisi tumekutuma wewe kwa Haki, kuwa ni mbashiri
na mwonyaji. Na hapana umma wowote ila ulipata mwonyaji kati yao.
25. Na wakikukanusha basi walikwisha wakanusha walio kuwa
kabla yao. Mitume wao waliwajia kwa dalili wazi wazi na kwa maandiko na Kitabu
chenye nuru.
26. Kisha nikawakamata walio kufuru. Basi kuchukia kwangu
kulikuwaje?
27. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka
mbinguni, na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima
imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana.
28. Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao
zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake
ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.
29. Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na
wakashika Sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku,
hao hutaraji biashara isiyo bwaga.
30. Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na
awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye
shukrani.
31. Na hayo tuliyo kufunulia kutoka Kitabuni ni Kweli yenye
kusadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni
Mwenye khabari na Mwenye kuona.
32. Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateuwa
miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliye jidhulumu nafsi yake, na yupo wa
katikati, na yupo aliye tangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.
33. Mabustani ya milele watayaingia. Huko watavikwa vikuku
vya dhahabu, na lulu, na nguo zao humo ni za hariri.
34. Na watasema: Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za
Mwenyezi Mungu aliye tuondolea huzuni zote. Hakika Mola wetu Mlezi bila ya
shaka ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani.
35. Ambaye kwa fadhila yake ametuweka makao ya kukaa daima;
humu haitugusi taabu wala humu hakutugusi kuchoka.
36. Na walio kufuru watakuwa na Moto wa Jahannamu,
hawahukumiwi wakafa, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyo
mlipa kila mwenye kuzidi ukafiri.
37. Na humo watapiga makelele: Mola wetu Mlezi! Tutoe
tufanye mema sio yale tuliyo kuwa tukiyafanya. Kwani hatukukupeni umri wa
kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka? Na akakujieni Mwonyaji? Basi onjeni! Kwani
walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
38. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa siri za mbinguni
na ardhi. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliomo vifuani.
39. Yeye ndiye aliye kufanyeni manaibu katika ardhi. Na
anaye kufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri
haziwazidishii kwa Mola wao Mlezi ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri
haziwazidishii ila khasara.
40. Sema: Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnao
waomba badala ya Mwenyezi Mungu! Nionyesheni wameumba sehemu gani katika ardhi?
Au wana ushirika wowote katika
mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na hoja zilizo wazi? Lakini
madhaalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu tu.
41. Hakika
Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka
hapana yeyote wa kuzizuia isipo kuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye
kusamehe.
42. Na waliapa
kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwajia mwonyaji bila ya shaka
watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipo wajia
mwonyaji hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo Haki,
43. Kwa
kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu
havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya. Hebu hawangojei yalio wasibu watu wa kale?
Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko
katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.
44. Je!
Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao?
Na hao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao. Na hapana kitu kinacho weza
kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye
kujua, Mwenye uweza.
45. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa waliyo yachuma, basi asingeli muacha
juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini Yeye anawachukulia mpaka ufike muda
maalumu. Basi ukifika muda wao basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona
waja wake baraabara.
|