36. SURAT YA-SIN
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanzia kwa
harufi mbili ambazo ni katika harufi za kuundiwa maneno ya Kiarabu. Na
ikafuatiliza kwa kuapa kwa Qur'ani ya kwamba Muhammad s.a.w. bila ya shaka ni
miongoni mwa Mitume, walio tumwa. Na kuwa hakika yeye yuko kwenye Njia Iliyo
Nyooka iliyo rasimiwa na Qur'ani aliyo teremshiwa yeye kutokana na Mtukufu
Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu, ili apate kuwaonya kwayo watu ambao baba zao
hawakupata kabla yake kuonywa. Tena Sura ikaingia kutufanyia taswira, picha, ya
wanao kataa, ambao hawanafiiki na maonyo. Na inatubainishia kwamba kuonya
humfaidisha mwenye kuelekea kupokea makumbusho, na kumcha Mwingi wa Rehema. Na
kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua wafu, na atavihisabu vitendo vya waja.
Na Sura ikaingilia kuwapigia mfano makafiri wa Makka, na ikabainisha mvutano
baina ya wanao mlingania Mwenyezi Mungu na wanao kadhibisha. Inabainisha mwisho
wa makundi mawili hayo. Kisha ikawa inaeleza dalili za uweza unao pasa kuuamini
na kuogopa miadi ya Mwenyezi Mungu itakayo watokea ghafla katika Siku ambayo
kila mtu atalipwa kwa aliyo yatenda. Watu wa Peponi watastareheshwa. Watapata
wanacho kitamani. Na watu wa Motoni watafukuzwa. Nao watakuwa katika mbano wa
uweza wa Mwenyezi Mungu. Midomo yao itazibwa, na viungo vyao ndivyo vitavyo
tamka. Na Mwenyezi Mungu angeli penda, basi bila ya shaka angeli zigeuza sura
zao pia. Kwani ni Yeye ndiye Mwenye kumbadilisha anaye mrefushia umri wake
duniani badala ya nguvu akawa dhaifu, na badala ya akili akawa amepiswa. Na
Yeye ndiye aliye mlinda Nabii wake na kuzugwa na kichaa. Naye hakumfundisha
utungaji mashairi, na wala hauhitajiki ufundi huo unao mfanya aliye nao kutanga
tanga katika kila bonde. Mtume hakuja ila kwa ajili ya ukumbusho ulio wazi,
ulio tokana na akili, sio ulio tokana na mawazo mapepe tu. Na Sura ikaendelea
kukumbusha fadhila za Mwenyezi Mungu juu ya waja wake, na kwamba Yeye
amewafanya wanyama wa mifugo ambao wanawamiliki na wanawapanda wawatumikie. Na
juu ya neema hizi zilio wekwa kwa faida yao, wao bado wanakwenda kuabudu miungu
ya ushirikina isiyo weza kitu. Na Sura inakhitimisha kwa kumtaka binaadamu
aangalie namna alivyo umbwa kutokana na tone la manii, na khalafu yeye anakuwa
ni mpinzani wa kudhihirisha upinzani wake. Na yule aliye umba hapo mwanzo, na
anaye toa moto kutoka mti wa kijani, na aliye umba mbingu na ardhi, huyo basi
ni Muweza wa kuyafufua mafupa nayo yamekwisha vurugika. Na amri yake ni
kukiambia kitu: Kuwa! Na kikawa. Ametakasika Mwenye kumiliki kila kitu. Na kwake Yeye mtarejea.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|