Table of Contents | Words: Alphabetical - Frequency - Inverse - Length - Statistics | Help | IntraText Library

Qu'rani

IntraText CT - Text

  • 37. SURAT ASS'AFFAT
Previous - Next

Click here to hide the links to concordance

37. SURAT ASS'AFFAT

(Imeteremka Makka)

Sura hii imeanza kwa kiapo kwa mataifa miongoni mwa viumbe vya Mwenyezi Mungu ambayo yana sifa ya kujipanga kwa safu, na kuzuia, na kusoma. Kiapo hicho ni kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Na Ishara zinashuhudia kwa hayo. Kwani Yeye ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, na Yeye ni Mola Mlezi wa mashariki na magharibi, ambaye aliye ipamba mbingu ya dunia kwa nyota, na akaifanya ihifadhike na muasi aliye acha ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Na baada ya kuthibitisha itikadi ya Tawhidi, Sura imeendelea kuthibitisha itikadi ya kufufuliwa. Na ikawahadharisha wenye kutia shaka kuwa huko kufufuliwa kutawazukia ghafla nao wanaona. Na ikazileta dalili za kumkinika huko, bali wepesi wa kutokea kwake, na hali wao wanayaona hayo na wanasema: Hii ndiyo Siku ya Hisabu! Na wataambiwa: Hii ndiyo Siku ya mpambanuo mlio kuwa mkiikanusha. Na watakusanywa madhaalimu na walivyo kuwa wakiviabudu. Na watasailiwa na watahojiwa. Na watakuwa wakisingiziana wao kwa wao madhambi walio yapata, na hali wote watakuwa wanashirikiana pamoja katika adhabu. Kwani walijivuna wakakataa kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, na wakamsingizia Mtume wao kuwa ana kichaa na wazimu; na hali kuwa hapana shaka kuwa kawajia na Haki. Na Mitume wamesema kweli katika waliyo kuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Waumini wenye ikhlasi watastareheshwa kwa kila namna ya neema. Na watazikumbuka neema za Mwenyezi Mungu. Watawatokea watu waovu, na watawaona katikati ya Moto wa Jahim. Watamhimidi Mwenyezi Mungu kwa alivyo walinda, na walivyo okoka wasifuate wito wa wale waovu. Baada ya hayo Sura ikaingia ikieleza mashukio ya walio dhulumu na mashukio ya Waumini. Tena ikafuatiliza kwa kueleza khabari za Mitume wengine ili kumpoza Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kuwapa mawaidha watu wake wanao pinga. Na baada ya hadithi mbali mbali za zama mbali mbali na watu mbali mbali, zilizo eleza cheo cha Ujumbe na Wajumbe wenyewe, Sura imetengua madai ya washirikina kwamba Mwenyezi Mungu ana mabinti na wao wana watoto wanaume. Na kwamba Yeye amewafanya Malaika ni wanawake. Na kwamba ipo nasaba ya kukhusiana baina yake na majini. Mwenyezi Mungu Ametakasika na hayo wanayo yazua. Na waja wake ndio watanusuriwa, na jeshi lake ndilo litakalo shinda. Na adhabu yake itaifanya ovu asubuhi ya wanao onywa. Na Sura ikakhitimisha kwa kumtakasa Mola Mlezi wa Utukufu na hayo wanayo mzulia. Na amani ishuke kwa Mitume wote, na Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU




Previous - Next

Table of Contents | Words: Alphabetical - Frequency - Inverse - Length - Statistics | Help | IntraText Library

Best viewed with any browser at 800x600 or 768x1024 on Tablet PC
IntraText® (V89) - Some rights reserved by EuloTech SRL - 1996-2007. Content in this page is licensed under a Creative Commons License