38. SURAT S'AAD
(Imeteremka
Makka)
Sura hii ni ya thalathini
na nane katika Sura za . Nayo
ni Sura ya Makka, na Aya zake ni 88.
Sura hii inatueleza namna ya inda ya washirikina waliyo kuwa wakiufanyia Wito
wa Nabii Muhammad s.a.w. na uhasidi wao kwa vile Mwenyezi Mungu alivyo mkirimu kwa
kumpa utukufu wa Utume, na kumteremshia Qur'ani. Basi inawajibu kwa yale mawazo
ya uwongo walio mnasibishia nayo. Na imebainisha kwamba yaliyo wapelekea
kuupiga vita Wito wake kama wafanyavyo si lolote ila ni dharau ya uwongo, na
kupenda kuleta khitilafu na mgawanyo. Na lau kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu inge
wateremkia, msimamo wao kwa Mtume s.a.w. usingeli kuwa hivyo ulivyo. Kisha
Mwenyezi Mungu amewapigia mifano ya kaumu zilizo kwisha tangulia, ili wapate
kuacha inadi na kuleta dhiki, na ili kumpa moyo Mtume wake s.a.w. kufikisha
Wito, na hata ange pata taabu zozote na vitimbi vyovyote vya washirikina kwa
ajili yake. Na apate kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema alizo mpa, kama
walivyo fanya ndugu zake Manabii na Mitume wengine. Na kutokea na haya anataja
marejeo mema aliyo waandalia Mwenyezi Mungu wachamngu, na maangukio maovu aliyo
waandalia wenye kuasi. Kisha akawakumbusha yaliyo kuwa baina ya baba yao Adam
a.s. na adui yake Iblisi, ili wajue kuwa anayo waitia Iblisi kufanya kiburi kwa
kupinga kufwata haki ni tabia katika tabia zake Iblisi. Na kupanda kiburi huku
ndiko kulikuwa sababu ya kufukuzwa kwake kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu.
Sura imekhitimisha kwa kueleza vilivyo kazi muhimu ya Mtume s.a.w., nayo ni
kufikisha Wito, na kwamba yeye hawataki ujira kwa hayo, na yeye hakujileta
nafsi yake. Na Qur'ani si chochote ila ni Ukumbusho kwa walimwengu wote. Na
bila ya shaka watakuja jua ukweli wa khabari zake baadae.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|