1 - 50
1. Mteremsho wa Kitabu hiki umetokana na Mwenyezi Mungu,
Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
2. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi
muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu.
3. Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanao
wafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate
kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu
baina yao katika wanayo khitalifiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi aliye
mwongo kafiri.
4. Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, basi
bila ya shaka angeli teua amtakaye katika alio waumba. Subhanahu, Ametakasika
na hayo! Yeye ni Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda atakalo.
5. Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Hufunika usiku juu ya
mchana, na hufunika mchana juu ya usiku. Na amefanya jua na mwezi vitumike.
Kila kimojapo kinakwenda kwa kipindi kilicho wekewa. Jueni mtanabahi! Yeye
ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe!
6. Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya
mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane.
Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza
vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi
nyinyi mnageuzwa wapi?
7. Mkikufuru
basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja
wake. Na mkishukuru Yeye hufurahika nanyi. Wala mbebaji habebi mzigo wa
mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi. Hapo atakwambieni mliyo
kuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyomo vifuani.
8. Na taabu
inapo mfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi naye ameelekea kwake. Kisha akimpa
neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa akimwitia zamani, na akamfanyia
Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu njia yake. Sema: Starehe na ukafiri
wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni.
9. Je! Afanyae
ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji
rehema za Mola wake Mlezi...Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale
wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili.
10. Sema: Enyi waja wangu mlio amini! Mcheni Mola wenu
Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi
Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
11. Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu
kwa kumsafishia Dini Yeye tu.
12. Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu.
13. Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya Siku Kubwa
nikimuasi Mola wangu Mlezi.
14. Sema: Mwenyezi Mungu tu namuabudu kwa kumsafishia Yeye
tu Dini yangu.
15. Basi nyinyi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Sema:
Hakika walio khasirika ni wale walio jikhasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya
Kiyama. Tambueni kuwa hiyo ndiyo khasara iliyo dhaahiri.
16. Yatawekwa juu yao mat'abaka ya moto, na chini yao
mat'abaka. Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawakhofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni Mimi!
17. Na wale wanao jiepusha na ibada potovu, na wakarejea
kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu.
18. Ambao husikiliza maneno, wakafuata lilio bora yao. Hao
ndio alio waongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili.
19. Je! Yule mwenye kustahiki hukumu ya adhabu, je, wewe
unaweza kumwokoa aliyomo katika Moto?
20. Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata ghorofa
zilizo jengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi
Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake.
21. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka
mbinguni. Kisha akayapitisha kwenye chemchem katika ardhi, kisha kwa maji hayo
akatoa mimea yenye rangi mbali mbali? Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano,
na kisha huifanya mapepe. Bila ya shaka katika hayo upo ukumbusho kwa wenye
akili.
22. Je! Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake
kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na
mwenye moyo mgumu?) Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisio mkumbuka Mwenyezi
Mungu! Hao wamo katika upotofu wa dhaahiri.
23. Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu
chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola
wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi
Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na
ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa.
24. Je! Atakaye kuwa anapambana kwa uso wake na adhabu
mbaya kabisa Siku ya Kiyama (ni sawa na watenda wema?) Na wataambiwa wenye
kudhulumu: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyachuma!
25. Walio kuwa kabla yao walikadhibisha , na ikawajia
adhabu kutoka pahala wasipo patambua.
26. Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai wa
duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangeli jua!
27. Na bila ya shaka tumewapigia watu mifano ya kila namna
katika hii Qur'ani ili wapate kukumbuka.
28. Qur'ani ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wamche Mungu.
29. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye mabwana
washirika wanao gombana, na wa mtu mwengine aliye khusika na bwana mmoja tu. Je! Wako sawa katika hali zao?
Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! Lakini wengi wao hawajui.
30. Kwa
hakika wewe utakufa, na wao watakufa.
31. Kisha
bila ya shaka mtagombana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu Mlezi.
32. BASI
NI NANI dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye msingizia uwongo Mwenyezi Mungu na
kuikanusha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika Jahannamu makaazi ya hao makafiri?
33. Na
aliye ileta Kweli na akaithibitisha - hao ndio wachamngu.
34.
Watapata watakacho taka kwa Mola wao Mlezi. Hayo ndiyo malipo ya watendao mema.
35. Ili
Mwenyezi Mungu awafutie ukomo wa uovu walio ufanya na awalipe ujira wao kwa
mujibu wa ukomo wa wema walio kuwa wakiutenda.
36. Je!
Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza mja wake? Na ati wanakutishia kwa hao
wenginewe wasio kuwa Yeye! Na aliye hukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea hana wa
kumwongoa.
37. Na
ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa hana wa kumpotoa. Je! Mwenyezi Mungu si Mwenye
nguvu anaye weza kulipiza?
38. Na
ukiwauliza: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi. Bila ya shaka watasema:
Mwenyezi Mungu. Sema: Je! Mnawaonaje wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu,
ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au
akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake? Sema: Mwenyezi
Mungu ananitosheleza. Kwake
Yeye wategemee wanao tegemea.
39. Sema:
Enyi watu wangu! Fanyeni mwezavyo, mimi pia nafanya. Basi mtakuja ona
40. Ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye
mshukia adhabu ya daima.
41. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu
wote kwa Haki. Basi mwenye kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila
ya shaka amepotoka kwa khasara yake. Na wewe si mlinzi juu yao.
42. MWENYEZI MUNGU huzipokea roho zinapo kufa. Na zile
zisio kufa wakati wa kulala kwake, huzishika zilizo hukumiwa kufa, na
huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya
shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
43. Au ndio wanachukua waombezi badala ya Mwenyezi Mungu?
Sema: Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote, wala hawatambui lolote?
44. Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Ni wake Yeye
tu ufalme wa mbingu na ardhi. Kisha mtarejeshwa kwake.
45. Na anapo tajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyoyo za wasio
iamini Akhera huchafuka. Na wanapo tajwa wenginewe asiye kuwa Yeye basi wao
hufurahi.
46. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba mbingu na ardhi! Mjuzi
wa yasiyo onekana na yanayo onekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika
waliyo kuwa wakikhitalifiana.
47. Na lau kuwa walio dhulumu wangeli kuwa na vyote viliomo
duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa
kujikomboa katika adhabu mbaya hiyo Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa
Mwenyezi Mungu wasiyo kuwa wakiyatarajia.
48. Na utawadhihirikia ubaya wa waliyo yachuma,
yatawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
49. Na dhara inapo mgusa mtu hutuomba. Kisha tunapo mpa
neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Sio! Huo
ni mtihani! Lakini wengi wao
hawajui!
50.
Waliyasema haya waliyo kuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyo kuwa
wakiyachuma.
|