40. SURAT GHAAFIR (AU AL MUUMIN)
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanzia, kama
zilivyo anzia Sura nyingi, kwa harufi mbili katika harufi za Alifbete. Na
ikaanza kwa kutaja shani ya Qur'ani iliyo teremka kutokana na Mwenye nguvu,
Mwenye ujuzi, Mwenye kusamehe madhambi, Mwenye kukubali toba, Mkali wa
kuadhibu, Mwenye ukarimu. Kisha ikaitia Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja,
na kuacha kudanganyika na utawala ambao huenda makafiri wakawa nao, na
ikawataka watu wakumbuke matokeo ya kaumu zilizo kuwa kabla yao.
Baada ya hayo Sura imesimulia khabari za wabebaji A'rshi, na kusabihi kwao, na
madua yao. Na ikaeleza hali ya makafiri, na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu juu yao.
Na Sura ikasimulia zaidi kuliko mara moja juu ya Ishara za Mwenyezi Mungu na
uwezo wake katika nafsi zao, na yaliyo wazunguka ya mbinguni na kwenye ardhi,
na neema zinazo wamiminikia, kama inavyo waitia katika zaidi kuliko Aya moja
wamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja kwa kumuabudu Yeye tu: "Basi mwombeni
Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu." "Na alisema Mola wenu
Mlezi: Niombeni, nitakuitikieni!" "Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola
wenu Mlezi Mungu, Muumba wa kila kitu. Hapana mungu isipo kuwa Yeye." Kama
vile vile Sura hii ilivyo kusanya katika baadhi ya Aya zake maneno ya
kukumbusha Siku ya Mwisho: "Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo
zitakapo fika kooni nao wamejaa huzuni." Na Sura imesimulia kidogo katika
kisa cha Musa a.s. pamoja na Firauni, na khasa walio amini katika watu wa
Firauni. Na Sura ikakhitimishia kwa kuwataka watu watembee katika ardhi waone
yaliyo wafika kaumu zilizo kuwako kabla yao, na vipi ulikuwa mwisho wa ghururi
zao kwa ilimu walizo kuwa nazo. Na ilipo wafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu walisema:
Tunamuamini Mwenyezi Mungu pekee, na tunawakanya hao miungu tuliyo kuwa
tukimshirikisha nao. Lakini hao wameamini baada ya kwisha pita wakati,
"Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa wakati ambao wamekwisha iona
adhabu yetu." Na huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake, wala
hutakuta mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu. Na inapo shuka adhabu hapo
ndipo watapo khasiri makafiri.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|