51 - 85
51. Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na
walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi,
52. Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao
watapata laana, na watapata makaazi mabaya kabisa.
53. Na kwa hakika tulimpa Musa uwongofu, na tukawarithisha
Wana wa Israili Kitabu,
54. Ambacho ni Uwongofu na Ukumbusho kwa wenye akili.
55. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli.
Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi
jioni na asubuhi.
56. Hakika hao wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi
Mungu bila ya uthibitisho wowote uliyo wajia, hawana vifuani mwao ila kutaka
ukubwa tu, na wala huo hawaufikilii. Basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika
Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
57. Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi
kuliko kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui.
58. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani; na walio amini
na watendao mema hawalingani na muovu. Ni machache mnayo yakumbuka.
59. Hakika Saa (ya Kiyama) itafika, nayo haina shaka.
Lakini watu wengi hawaamini.
60. Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni.
Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu
wadhalilike.
61. Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni usiku ili mpate kutulia
humo, na mchana wa kuonea. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye
fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.
62. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi, Muumba wa
kila kitu. Hapana mungu ila Yeye; basi mnageuzwa wapi?
63. Namna hivi ndivyo walivyo geuzwa walio kuwa wakizikataa
Ishara za Mwenyezi Mungu.
64. Ni Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni ardhi kuwa ni pahala
pa kukaa, na mbingu kuwa dari. Na akakutieni sura, na akazifanya nzuri sura
zenu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi.
Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.
65. Yeye ndiye aliye Hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye.
Basi muabuduni Yeye mkimsafishia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi
Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
66. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala
ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja zilizo dhaahiri kutokana na Mola wangu
Mlezi. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote.
67. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la
manii, kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga,
kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo
wanao kufa kabla, na ili mfikie muda ulio kwisha wekwa, na ili mpate kufahamu.
68. Yeye
ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa!
Likawa.
69. Je!
Huwaoni wale wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu? Wanageuziwa wapi?
70. Ambao
wamekanusha Kitabu na yale tuliyo watuma Mitume wetu. Basi watakuja jua.
71.
Zitakapo kuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa
72. Katika
maji ya moto, kisha wanaunguzwa Motoni,
73. Tena
wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwashirikisha
74. Badala
ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea, bali tangu zamani hatukuwa tukiomba
kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawaachia makafiri wapotelee mbali.
75. Haya
ni kwa sababu mlikuwa mkijitapa katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa
mkijishaua.
76.
Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo milele. Basi ni maovu yaliyoje
makaazi ya wanao takabari!
77. Basi
subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na ama tukikuonyesha baadhi
ya yale tuliyo waahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu.
78. Na
bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia
khabari zao, na wengine hatukukusimulia. Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila
kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Basi ikija amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa
Haki, na hapo wapotofu watakhasiri.
79.
Mwenyezi Mungu aliye kujaalieni nyama hoa, mifugo, ili muwapande baadhi yao, na
muwale baadhi yao.
80. Na
katika hao mnayo manufaa kadhaa wa kadhaa, na mnapata kwao haja ziliomo vifuani
mwenu; na mnachukuliwa juu yao, na juu ya marikebu.
81. Naye
anakuonyesheni Ishara zake. Basi Ishara gani za Mwenyezi Mungu mnazo zikataa?
82. Kwani
hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa walio kuwa kabla yao? Wao
walikuwa wengi kuliko hawa, na wamewashinda kwa nguvu na athari katika nchi.
Wala hayakuwafaa hayo waliyo kuwa wakiyachuma.
83. Walipo
wajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi walijitapa kwa ilimu waliyo kuwa nayo.
Basi yakawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia maskhara.
84. Walipo
iona adhabu yetu walisema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni wa pekee, na
tunaikataa miungu tuliyo kuwa tukiishirikisha naye.
85. Lakini
imani yao haikuwa yenye kuwafaa kitu wakati ambao wamekwisha iona adhabu yetu.
Huu ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kuwa kwa waja wake. Na hapo walio kufuru
walikhasiri.
|