42. SURAT ASH-SHUURA
(Imeteremka
Makka)
Hii ni Sura ya Makka, na
idadi ya Aya zake ni 53, na imeitwa Ash-shuura, yaani "Kushauriana"
kwa sababu inavyo waongoza Waumini waendeshe mambo ya jamii zao kwa
kushauriana, ili ipatikane Haki, na uthibiti uadilifu. Na Sura hii
imekusanya mambo mengi ya Dini na hoja za itikadi.
Imefungua Sura kwa kuisifu Qur'ani yenyewe kwa kuwa ni Wahyi (Ufunuo) ulio toka
kwa Mwenyezi Mungu, ikayarudisha matusi ya makafiri, na ikashughulikia kumpoza
Mtume s.a.w., na tena baada ya hayo ikaingilia kuthibitisha uweza wa Mwenyezi
Mungu aliye iteremsha Qur'ani na ukatukuka utawala wake, na ikaeleza kukanya
kwa baadhi ya watu juu ya kuwa hoja zake ziwazi zinazo onyesha kuwa haya
yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kubainisha khitilafu zao katika kufahamu Haki.
Na baada yake Sura hii ikatilia mkazo uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya
kila kitu. Kisha ikathibitisha kuwa msingi wa sharia ni mmoja, na ikaashiria
kuwa wapo wanao kufuru juu ya hivyo. Hali kadhaalika imeashiria kuwa Vitabu
vyote vya mbinguni vinaongoza kwendea Haki. Na Sura imelaani shirki ya
washirikina, na kukhitalifiana kwao katika Haki kwa udhalimu tu. Na pia
imelaani kule kuhimiza kwao, wanao kadhibisha, kuhimiza Kiyama kwa maskhara. Na
ikatoa uwongozi kwa wafuasi wake wawalinganie watu kwenye Dini, kama ilivyo
eleza ubora wa upole wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na Sura hii imehadharisha
kuzama katika kuiwania dunia tu peke yake. Na ikabainisha uovu wa hali ya
makafiri na wema wa hali ya Waumini katika Akhera. Na Sura ikawalaumu wale
walio mkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kwa kumwambia kaizua Qur'ani,
hali wao wameshindwa hata kuleta Sura moja tu mfano wake. Kisha ikatangaza kuwa
Mwenyezi Mungu ameikubali toba ya Waumini, na ikatangaza hikima ya kuzigawa
riziki kwa watu kwa mpango wa hikima. Hawakuwa wote matajiri, kwa kuchelea
wasipande jeuri, wala wasiwe wote mafakiri wakateketea. Bali amewakunjulia
baadhi na amewadhikisha wengine.
Na akadhihirisha baraka za mvua, na dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kwa jambo
hili, na kwamba masaibu ya dunia ni kwa sababu ya maasi. Kisha Subhanahu
akakariri kwa njia nyingine hali za Waumini na wanao kadhibisha huko Akhera, na
madhila yatayo wapata wanao kadhibisha. Na akataka wafanye haraka kuitikia wito
wa Mwenyezi Mungu kabla uhai haujakata fursa ya kutenda. Kadhaalika Sura
imeshughulika kumpoza Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. na kubainisha uweza wake
Subhanahu kumtunukia amtakaye watoto wa kike, na wa kiume mwenginewe, na
mchanganyiko kwa wa tatu, na kumnyima kabisa wa nne. Kisha Sura ikataja njia za
Mwenyezi Mungu kusema na Manabii wake, na ikakhitimisha kwa kubainisha Njia ya
Haki Iliyo Nyooka ambayo inayo pasa kuifuata.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. H'a Mim
2. A'yn
Sin Qaf
3. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye hikima
anavyo kuletea Wahyi wewe na walio kabla yako.
4. Ni vyake viliomo mbinguni, na viliomo katika ardhi. Na
Yeye ndiye Mtukufu, Mkuu.
5. Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa
Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
6. Na wale walio wafanya walinzi wengine badala yake Yeye,
Mwenyezi Mungu ni Mwangalizi juu yao. Wala wewe si wakili juu yao.
7. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili
uwaonye watu wa Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku
ya Mkutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine
Motoni.
8. Na Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote umma
mmoja, lakini anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu
hawana mlinzi wala msaidizi.
9. Au
wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi
khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza wa kila kitu.
10. Na
mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu.
Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye mtegemea na kwake Yeye
narejea.
11. Yeye
ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na
katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama
mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
12. Yeye
ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki amtakaye, na
humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu.
13.
Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na
tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane
kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi Mungu humteua
kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye.
14. Na
hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya husuda iliyo kuwa baina
yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola wako Mlezi ya
kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka palingeli hukumiwa baina
yao. Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka inayo
wahangaisha.
15. Basi
kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wala usiyafuate
matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha Mwenyezi Mungu katika
Vitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni Mola
wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo vyetu, na nyinyi
mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu na nyinyi. Na
Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.
16. Na wanao hojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya
kukubaliwa, hoja za hawa ni baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo
ghadhabu, na itakuwa kwao adhabu kali.
17. Mwenyezi Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu kwa Haki, na
Mizani. Na nini kitakacho kujuulisha ya kwamba pengine Saa ya Kiyama ipo
karibu?
18. Wasio amini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini
wanao amini wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika
hao wanao bishana katika khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali
kabisa.
19. Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake. Humruzuku
ampendaye. Naye ni Mwenye nguvu, Mtukufu.
20. Mwenye kutaka mavuno ya Akhera tutamzidishia katika
mavuno yake, na mwenye kutaka mavuno ya duniani tutampa katika hayo, lakini
katika Akhera hana fungu.
21. Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia dini
asiyo itolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisinge kuwako neno la kupambanua
basi wangeli katiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu
chungu.
22. Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa
sababu ya waliyo yachuma, nayo yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema
watakuwamo katika mabustani ya Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao
Mlezi. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.
23. Hayo ndiyo aliyo wabashiria Mwenyezi Mungu waja wake
walio amini na wakatenda mema. Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi
katika kujikurubisha. Na anaye fanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Msamehevu Mwenye shukrani.
24. Ati wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi
Mungu akipenda atapiga muhuri juu ya moyo wako. Na Mwenyezi Mungu anaufuta
upotofu na anaithibitisha Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua yaliomo
vifuani.
25. Naye ndiye anaye pokea toba kwa waja wake, na anasamehe
makosa, na anayajua mnayo yatenda.
26. Na anawaitikia wanao amini na wakatenda mema, na
anawazidishia fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu chungu.
27. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki
waja wake, basi bila ya shaka wangeli panda kiburi katika dunia. Lakini
anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na
anawaona.
28. Naye ndiye anaye iteremsha mvua baada ya wao kwisha
kata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Mlinzi Mwenye kuhimidiwa.
29. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na
wanyama alio waeneza. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo.
30. Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya
mikono yenu. Naye anasamehe mengi.
31. Na nyinyi
hamwezi kushinda katika ardhi. Na wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi badala
ya Mwenyezi Mungu.
32. Na katika Ishara
zake ni vyombo vinavyo kwenda na kurejea baharini kama vilima.
33. Akitaka,
huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika
hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
34. Au
huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyo yatenda hao watu. Naye husamehe
mengi.
35. Na ili wajue
wanao jadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia.
36. Basi vyote
mlivyo pewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi
Mungu ni bora, na cha kudumu kwa ajili ya walio amini, na wakawa wanamtegemea
Mola wao Mlezi,
37. Na wanayo
yaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapo kasirika wao husamehe,
38. Na wanao
mwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na mambo yao yakawa ni kwa
kushauriana baina yao, na kutokana na tulicho waruzuku wakawa wanatoa,
39. Na ambao
wanapo fanyiwa jeuri hujitetea.
40. Na malipo ya
uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo
malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.
41. Na wanao
jitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu.
42. Bali lawama
ipo kwa wale wanao wadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika nchi bila ya haki.
Hao watapata adhabu iliyo chungu.
43. Na anaye
subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.
44. Na ambaye Mwenyezi
Mungu amemwacha kupotea, hana mlinzi baada yake. Na utawaona wenye kudhulumu
watakapo iona adhabu wanasema: Je! Ipo njia ya kurudi?
45. Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea
kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walio amini watasema: Hakika
wapatao khasara ni hao walio khasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ama
hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya daima.
46. Wala hawatakuwa na walinzi wa kuwanusuru mbele ya
Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana njia yoyote.
47. Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku isiyo
epukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa pa kukimbilia wala
hamtakuwa na cha kukingia.
48. Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe
mwangalizi wao. Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi
tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa
sababu ya iliyo yatanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.
49. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba
apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto
wa kiume,
50. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya
amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.
51. Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu
amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye
humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.
52. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa amri yetu.
Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru
ambayo kwayo tunammwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa
kwenye Njia Iliyo Nyooka.
53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu viliomo
mbinguni na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.
|