44. SURAT ADDUKHAN
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanza kwa
kusimulia khabari za Qur'ani, ya kwamba imeteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu
katika usiku wa Lailatul Qadri ulio barikiwa, kwa ajili ya kuonya na Tawhid,
Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Na kwamba hii Qur'ani ni Haki, Kweli tupu. Hali
kadhaalika Sura imesimulia khabari za kufufuliwa, na kwamba hayo hayana shaka
ndani yake, na imezibisha hoja za wanao yakanya hayo, na ikawarudi washirikina.
Ikalinganisha baina ya washirikina wa Makka na wenzao walio watangulia, nao ni
kaumu ya Firauni. Ikaeleza mapatilizo ya Mwenyezi Mungu yaliyo washukia hao.
Tena ikatilia mkazo kwamba Siku ya Kiyama ndiyo siku iliyo pangwa ya kuutenga
ukafiri na upotovu wote. Na ikasimulia malipo ya wakosefu kwa siku hiyo na
malipo ya walio ongoka. Na ikamalizika kama ilivyo anzia kwa mazungumzo juu ya
Qur'ani, na kwa kuwaonya wanao kadhibisha Ujumbe wa Mtume s.a.w. kuwa nao
wangojee balaa na masaibu yatakayo washukia.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. H'a Mim
2. Naapa
kwa Kitabu kinacho bainisha,
3. Hakika
tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji.
4. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima,
5. Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.
6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni
Mwenye kusikia Mwenye kujua.
7. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa
nyinyi mna yakini.
8. Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi
wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.
9. Lakini wao wanacheza katika shaka.
10. Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio
dhaahiri,
11. Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu!
12. Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika
tutaamini.
13. Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia
Mtume mwenye kubainisha.
14. Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa,
naye ni mwendawazimu.
15. Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa
yakini mtarejea vile vile!
16. Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya
shaka Sisi ni wenye kutesa.
17. Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa
Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu.
18. Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi
kwenu ni Mtume Muaminifu.
19. Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi
nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi.
20. Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu
Mlezi pia, ili msinipige mawe.
21. Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.
22. Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni
wakosefu.
23. Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku.
Kwa yakini mtafuatwa.
24. Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni
jeshi litakalo zamishwa.
25. Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!
26. Na mimea na vyeo vitukufu!
27. Na
neema walizo kuwa wakijistareheshea!
28. Ndio
hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe.
29. La
mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula.
30. Na
bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha,
31. Ya
Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka.
32. Na
tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe.
33. Na
tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.
34. Hakika
hawa wanasema:
35. Hapana
ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi.
36. Basi
warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
37. Je! Ni
wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao
walikuwa wakosefu.
38. Na
hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo.
39.
Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.
40. Hakika
siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote.
41. Siku
ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.
42. Isipo
kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye
kurehemu.
43. Hakika
Mti wa Zaqqum,
44. Ni
chakula cha mwenye dhambi.
45. Kama
shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni
46. Kama
kutokota kwa maji ya moto.
47.
(Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu!
48. Kisha mmwagieni
juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka.
49. Onja!
Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!
50. Hakika
haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka.
51. Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani,
52. Katika mabustani na chemchem,
53. Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana,
54. Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini.
55. Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.
56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na
(Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu,
57. Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
58. Basi
tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.
59. Ngoja tu, na wao wangoje pia.
|