47. SURAT MUH'AMMAD
(Imeteremka
Madina)
Sura hii imeanza mwanzo wake
kubainisha kwamba Mwenyezi Mungu amezibat'ilisha a'mali za makafiri kwa kuwa
wamefuata upotovu, na amewafutia Waumini maovu yao kwa kufuata kwao Haki. Kama
ilivyo eleza kwa urefu waajibu wa kuitetea Haki. Na malipo hayo kwa Akhera ni
kuingia Peponi. Na ikawahimiza Waumini wainusuru Dini ya Mwenyezi Mungu na
wapigane kwa ajili yake. Na imeweka wazi kwamba wapotovu wakiacha Imani hufanya
fisadi katika nchi na wakawatupa jamaa zao. Na inahadharisha juu ya wanaafiki
kuwa pamoja na Waumini wakapeleleza siri zao wapate kuwavunja moyo. Na
inawatishia wanaafiki kuwa yatachanwa mapazia yao wanayo jifichia, na Mtume wa
Mwenyezi Mungu adhihirishe chuki zao. Na inawakataza Waumini wasiwe wanyonge
katika kupambana na makafiri, na hali wao ndio watakao shinda, na Mwenyezi
Mungu yu pamoja nao, na wala hatawanyima malipo ya kazi yao. Kisha Sura
imekhitimisha kutaka watu watoe kwa sababu ya Sabili Llah, Njia ya Mwenyezi
Mungu, na ikabainisha kwamba mwenye kufanya ubakhili katika hayo basi
anajidhuru mwenyewe, na kwamba kuacha kufuata Haki inakuwa ndiyo sababu ya
kuhiliki hao wenye kuacha na kuletwa kaumu nyengine zenye kuleta kheri.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Walio kufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, Yeye
atavipotoa vitendo vyao.
2. Na walio amini, na wakatenda mema, na wakaamini aliyo
teremshiwa Muhammad - nayo ni Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi - atawafutia
makosa yao na ataitengeneza hali yao.
3. Hayo ni kwa sababu walio kufuru wamefuata upotovu, na
walio amini wamefuata Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi. Hivyo ndivyo Mwenyezi
Mungu anavyo wapigia watu mifano yao.
4. Basi mnapo wakuta walio kufuru wapigeni shingoni mwao,
mpaka mkiwadhoofisha wafungeni pingu. Tena waachilieni kwa hisani au
wajikomboe, mpaka vita vipoe. Ndio hivyo. Na lau angeli taka Mwenyezi Mungu
angeli washinda mwenyewe, lakini haya ni kwa sababu akutieni mitihani nyinyi
kwa nyinyi. Na walio uliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu hatazipoteza a'mali
zao.
5. Atawaongoza na awatengezee hali yao.
6. Na atawaingiza katika Pepo aliyo wajuulisha.
7. Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye
atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.
8. Na walio kufuru, basi kwao ni maangamizo, na atavipoteza
vitendo vyao.
9. Hayo ni kwa sababu waliyachukia aliyo yateremsha
Mwenyezi Mungu, basi akaviangusha vitendo vyao.
10. Kwani hawakutembea katika ardhi wakaona ulikuwaje
mwisho wa walio kuwa kabla yao? Mwenyezi Mungu aliwaangamiza, na kwa makafiri
hawa itakuwa mfano wa hayo.
11. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio
amini. Na makafiri hawana mlinzi.
12. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na
wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Na walio kufuru
hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makaazi yao.
13. Na miji mingapi iliyo kuwa na nguvu zaidi kuliko mji
wako huu ulio kutoa; nao tuliwateketeza na wala hawakuwa wa kuwanusuru.
14. Je! Mwenye kuwa na bayana kutoka kwa Mola wake Mlezi ni
kama aliye pambiwa uovu wa vitendo vyake, na wakafuata pumbao lao?
15. Mfano wa Pepo walio ahidiwa wachamngu ina mito ya maji
yasiyo vunda, na mito ya maziwa isiyo haribika ladha yake, na mito ya mvinyo yenye
ladha kwa wanywao, na mito ya asali iliyo safishwa. Na wao humo watakuwa na
kila namna ya matunda, na maghfira kutoka kwa Mola wao Mlezi. Basi hao ni kama
watakao dumu Motoni na wakinyweshwa maji yanayo chemka ya kuwakata matumbo yao?
16. Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza, mpaka
wakiondoka kwako huwauliza walio pewa ilimu: Amesema nini sasa hivi? Hao ndio
ambao Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao, na wakafuata pumbao lao.
17. Na wale walio ongoka anawazidishia uongofu na anawapa
uchamngu wao.
18. Kwani wanangojea jengine isipo kuwa iwafikie Saa (ya
Kiyama) kwa ghafla? Na hakika alama zake zimekwisha kuja. Na itapo wajia
kutawafaa wapi kukumbuka hapo?
19. Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na
omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na
Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi, na mahali penu pa kukaa.
20. Na Waumini wanasema: Kwa nini haiteremshwi Sura? Na
inapo teremshwa Sura madhubuti na ikatajwa ndani yake khabari ya vita, utawaona
wenye maradhi katika nyoyo zao wanakutazama mtazamo wa anaye zimia kwa mauti.
Basi ni bora kwao
21. Ut'iifu na kauli njema. Na jambo likisha azimiwa, basi wakiwa
ni wakweli kwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka itakuwa ni kheri kwao.
22. Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi
katika nchi na mwatupe jamaa zenu?
23. Hao ndio Mwenyezi Mungu alio walaani, na akawatia
uziwi, na akawapofoa macho yao.
24. Je! Hawaizingatii hii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao)
zipo kufuli?
25. Kwa hakika wanao rudi nyuma baada ya kwisha wabainikia
uwongofu, Shetani huyo amewashawishi na amewaghuri.
26. Hayo ni kwa sababu waliwaambia walio chukia aliyo
yateremsha Mwenyezi Mungu: Tutakut'iini katika baadhi ya mambo. Na Mwenyezi
Mungu anajua siri zao.
27. Basi itakuwaje Malaika watakapo wafisha wakawa
wanawapiga nyuso zao na migongo yao!
28. Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yaliyo mchukiza
Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayo mridhisha, basi akaviangusha vitendo vyao.
29. Je! Wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba
Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?
30. Na tungeli penda tungeli kuonyesha hao na ungeli
watambua kwa alama zao; lakini bila ya shaka utawajua kwa namna ya msemo wao.
Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu.
31. Na bila ya shaka tutakujaribuni mpaka tuwadhihirishe
wapignao Jihadi katika nyinyi na wanao subiri. Nasi tutazifanyia mtihani
khabari zenu.
32. Kwa hakika walio kufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi
Mungu na wakapinzana na Mtume baada ya kwisha wabainikia uwongofu, hao
hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote. Naye ataviangusha vitendo vyao.
33. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini
Mtume, wala msiviharibu vitendo vyenu.
34. Hakika walio kufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi
Mungu, kisha wakafa na hali ni makafiri, Mwenyezi Mungu hatawasamehe makosa
yao.
35. Basi msiregee na kutaka suluhu, maana nyinyi ndio
mtakao shinda. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi, wala hatakunyimeni malipo ya
vitendo vyenu.
36. Hakika uhai wa duniani ni mchezo na pumbao. Na mkiamini
na mkamchamngu Mwenyezi Mungu atakupeni ujira wenu, wala hakutakeni mali yenu.
37. Na akikutakeni hayo na kukushikilieni mtafanya
ubakhili, na atatoa undani wa chuki zenu.
38. Angalieni! Nyinyi mnaitwa mtumie katika njia ya
Mwenyezi Mungu, na wapo katika nyinyi wanao fanya ubakhili. Na anaye fanya
ubakhili basi anajifanyia ubakhili mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu si mhitaji, na
nyinyi ndio wahitaji. Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao
hawatakuwa kama nyinyi.
|