48. SURAT AL FAT-H'I
(Imeteremka
Madina)
Imeanzia mwanzo wake Sura
hii kwa kutaja Ushindi ulio wazi, alio msahilishia Mwenyezi Mungu Mtume wake,
na imeelezea athari zake kubwa katika kueneza Uislamu na kuwatukuza Waislamu,
na kuziimarisha nyoyo za Waumini ili wazidi Imani, na kuadhibiwa kwa wanaafiki
na washirikina, kwa shaka shaka zao juu ya nusura ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume
wake. Na imetaja kuwa Mtume Muhammad s.a.w. ametumwa kuwa ni mwenye kushuhudia,
na mwenye kubashiria, ili ithibiti Imani ya Mwenyezi Mungu. Tena Sura ikaingia
kueleza kusimulia kuungwa mkono Mtume na watu wa kweli wa kutimiza ahadi, na
ikabainisha uwongo wa udhuru walio toa walio kwenda kinyume na Mtume wasitoke
naye kwenda pambana na maadui, na ambao walibaki nyuma kwa kudhania kwao kuwa
Mwenyezi Mungu hatampa nusura Mtume, na ikaeleza kuwa kutaka kwao kutoka naye
ni kwa sababu ya kupata ngawira.
Tena Sura imebainisha kuwa watakuja takiwa kupigana na kaumu wakali na wenye
nguvu, na kwamba hapana makosa kuacha kwenda vitani kwa udhuru wa kweli. Kama
ilivyo weka wazi ukubwa wa kheri alizo waahidi Mwenyezi Mungu wale alio furahi
nao katika kumuunga mkono Mtume s.a.w. kwa Ridhwani. Imezungumzia juu ya
kukimbia kwao makafiri na kushindwa kwao walipo pigana na Waumini, ikaeleza
hikima ya Mwenyezi Mungu kuwazuia makafiri wasiwapige Waumini, na kuwazuia
Waumini wasiwapige makafiri wakati wa kutekwa Makka. Na mazungumzo
yakamalizikia kwa kubainisha kwamba Mwenyezi Mungu ameitimiza ndoto aliyo iota
Mtume wake ya kuingia katika Msikiti Mtakatifu, na kwamba Muhammad na walio
amini pamoja naye ni wakali kwa makafiri lakini ni wapole, wanaoneana huruma
wao kwa wao. Na ikabainisha alama za kuwajuulisha Waumini, na sifa zao katika
Taurati na sifa zao katika Injili, na Mwenyezi Mungu kawaahidi walio amini na
wakatenda mema msamaha mkunjufu, na ujira mkubwa.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Hakika tumekufungulia Ushindi wa dhaahiri
2. Ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyo tangulia
na yajayo, na akutimizie neema zake, na akuongoe katika Njia Iliyo Nyooka,
3. Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu -
4. Yeye ndiye aliye teremsha utulivu katika nyoyo za
Waumini ili wazidi Imani juu ya Imani yao. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye
majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima -
5. Ili awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake katika
Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo, na awafutie makosa yao. Na huko
ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
6. Na awape adhabu wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake,
na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanao mdhania Mwenyezi Mungu
dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na
awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa.
7. Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
8. Hakika tumekutuma wewe uwe Shahidi, na Mbashiri, na
Mwonyaji,
9. Ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
mumsaidie, na mumhishimu, na mumtakase asubuhi na jioni.
10. Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika
wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao.
Basi avunjaye ahadi hizi anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza
aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.
11. Watakuambia mabedui walio baki nyuma: Yametushughulisha
mali yetu na ahali zetu, basi tuombee msamaha. Wanasema kwa ndimi zao yasiyo
kuwamo katika nyoyo zao. Sema: Ni nani awezaye kukusaidieni chochote kwa
Mwenyezi Mungu akitaka Yeye kukudhuruni au akitaka kukunufaisheni? Bali
Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
12. Lakini mlidhani kwamba Mtume na Waumini hawatarudi
kabisa kwa ahali zao, na mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu, na mkadhania dhana
mbaya, na mkawa watu wanao angamia.
13. Na asiye muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kwa
hakika Sisi tumewaandalia makafiri Moto mkali.
14. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye ufalme wa mbingu na
ardhi. Humsamehe amtakaye, na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
15. Walio baki nyuma watasema: Mtapo kwenda kuchukua
ngawira, tuacheni tukufuateni! Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu.
Sema: Hamtatufuata kabisa. Mwenyezi Mungu alikwisha sema kama hivi zamani. Hapo
watasema: Bali nyinyi mnatuhusudu. Siyo, bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.
16. Waambie walio achwa nyuma katika mabedui: Mtakuja itwa
kwenda pigana na watu wakali kwa vita, mpigane nao au wasalimu amri. Basi
mkimt'ii, Mwenyezi Mungu atakupeni ujira mzuri. Na mkigeuka kama mlivyo geuka
kwanza, atakuadhibuni kwa adhabu iliyo chungu.
17. Kipofu hana lawama, wala kiguru hana lawama, wala
mgonjwa hana lawama. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
atamuingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Na atakaye geuka upande
atamuadhibu kwa adhabu chungu.
18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo
fungamana nawe chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha
utulivu juu yao, na akawalipa kwa Ushindi wa karibu.
19. Na ngawira nyingi watakazo zichukua. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
20. Mwenyezi Mungu anakuahidini ngawira nyingi mtakazo
zichukua, basi amekutangulizieni hizi kwanza, na akaizuia mikono ya watu
isikufikieni, na ili hayo yawe ni Ishara kwa Waumini, na akakuongozeni Njia
Iliyo Nyooka.
21. Na mengine hamwezi kuyapata bado, Mwenyezi Mungu
amekwisha yazingia. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
22. Na lau makafiri wangeli pigana nanyi basi bila ya shaka
wangeli geuza migongo, kisha wasingeli pata mlinzi wala msaidizi.
23. Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kwisha pita
zamani, wala hutapata mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.
24. Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono
yenu kwao, katika bonde la Makka baada ya kukupeni Ushindi juu yao. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.
25. Hao ndio walio kufuru na wakakuzuieni msiingie Msikiti
Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao. Na lau si wanaume Waumini
na wanawake Waumini msio wajua mkawasaga na mkaingia makosani kutokana nao bila
ya kujua ...Mwenyezi Mungu (amefanya haya) ili amuingize amtakaye katika rehema
yake. Lau wangeli tengana bila ya shaka tungeli waadhibu walio kufuru kwa
adhabu chungu.
26. Pale walio kufuru walipo tia katika nyoyo zao hasira,
hasira za kijinga, Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu
ya Waumini, na akawalazimisha neno la kuchamngu. Na wao walikuwa ndio wenye
haki nalo na wenye kustahili. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
27. Hakika Mwenyezi Mungu amemtimizia Mtume wake ndoto ya
haki. Bila ya shaka nyinyi mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani,
na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza nywele. Hamtakuwa na khofu. Yeye
anajua msiyo yajua. Basi atakupeni kabla ya haya Ushindi karibuni.
28. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini
ya Haki, ili aitukuze juu ya dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa
Shahidi.
29. Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja
naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona
wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao
zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati.
Na mfano wao katika Injili ni kama mmea ulio toa chipukizi lake, kisha ukalitia
nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima,
ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini
na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.
|