59. SURAT AL-H'ASHRI
(Imeteremka
Madina)
Sura imeanzia kwa kutoa
khabari kwamba kila kitu kilioko katika mbingu na ardhi kinamsabihi na
kinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila kitu ambacho si laiki naye. Na kwamba Yeye
ni Mtukufu Mwenye nguvu asiye shindika, ni Mwenye hikima katika kuendesha kwake
na kupanga kwake Sharia. Na katika matokeo ya nguvu zake na hikima yake ni yale
yanayo simuliwa na Sura hii yaliyo wapata Bani Nnadhiiri, nao ni katika
Mayahudi wa Madina. Walikuwa hao walisuluhiana na Mtume s.a.w. baada ya kuhamia
Madina kwamba wasiwe dhidi yake wala upande wake. Walipo shindwa Waislamu
katika vita vya Uhud, walivunja agano lao wakaungana na Maqureshi dhidi ya
Mtume s.a.w. Hapo ndipo akenda akwazunguka katika ngome zao ambazo walidhani wenyewe
kuwa zitawalinda, na zisiweze kuwalinda. Tena ndio akawafukuza kutoka
Madina. Kisha Sura inaeleza hukumu ya mali yaliyo patikana kwa maadui bila ya
kupigana vita wala kukimbilia kwa farasi na kadhaalika. Ikataja kuwa hayo ni ya
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri,
na mafakiri katika wakimbizi walio tolewa kwenye nyumba zao na mali yao. Kisha
Sura ikasimulia khabari za Ansari, Waislamu wa Madina, na fadhila yao, na jinsi
walivyo kuwa wanawafadhilisha Wahajiri, wakimbizi, kuliko nafsi zao, ijapo kuwa
wao wenyewe wana haja ya hivyo wanavyo toa. Na Sura inataka macho yaangalie
zile ahadi za wanaafiki kwa Bani Nnadhiiri, na kauli yao waliyo sema: Pindi
mkitolewa, nasi tutatoka pamoja nanyi! Na mkipigwa vita tutakusaidieni! Basi
Sura imeufedhehi uwongo wao huo, udanganyifu wao katika hayo.
Kisha Sura ikamalizikia kwa kuwakumbusha Waumini kwa yatakikanayo wawe nayo,
nayo ni kumcha Mwenyezi Mungu, na kujiwekea akiba kwa siku zijazo za karibuni
na za mbali. Na wala wasiwe kama wale walio mpuuza Mwenyezi Mungu, naye
akawasahaulisha nafsi zao.
Na ikakhitimisha Sura kwa kubainisha hadhi ya Qur'ani na ubora wa taathira
yake. Hayo ni hivyo kwa sababu aliye iteremsha ni Yeye Mwenyezi Mungu ambaye
hapana mungu isipo kuwa Yeye Mwenye Asmau-l-H'usna, Majina Mazuri kabisa.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Vinamsabihi, Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika
mbingu na viliomo katika ardhi. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
2. Yeye ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa
Kitabu katika nyumba zao wakati wa uhamisho wa kwanza. Hamkudhani kuwa
watatoka, nao walidhani kuwa ngome zao zitawalinda na Mwenyezi Mungu. Lakini
Mwenyezi Mungu aliwafikia kwa mahali wasipo patazamia, na akatia woga katika
nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini.
Basi zingatieni enyi wenye macho!
3. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu asingeli waandikia kutoka,
angeli waadhibu katika dunia. Na katika Akhera watapata adhabu ya Moto.
4. Hayo ni kwa sababu walimpinga Mwenyezi Mungu na Mtume
wake. Na mwenye kumpinga Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa
kuadhibu.
5. Mtende wowote mlio ukata au mlio uacha unasimama vile
vile juu ya mashina yake, basi ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kwa kuwahizi
wapotovu.
6. Na mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka
kwao hamkuyakimbilia mbio kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa
mamlaka Mitume wake juu ya wowote awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya
kila kitu.
7. Mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa
watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya Mtume, na
jamaa, na mayatima, na masikini, na msafiri, ili yasiwe yakizunguka baina ya
matajiri tu miongoni mwenu. Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho
kukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mkali wa kuadhibu.
8. Wapewe mafakiri Wahajiri walio tolewa majumbani mwao na
mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake,
na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli.
9. Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao,
wanawapenda walio hamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo
pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni
wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye
kufanikiwa.
10. Na walio kuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi!
Tughufirie sisi na ndugu zetu walio tutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani
ya nyoyo zetu undani kwa walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na
Mwenye kurehemu.
11. Huwaoni wanao fanya unaafiki wanawaambia ndugu zao
walio kufuru katika Watu wa Kitabu: Mkitolewa na sisi lazima tutatoka pamoja
nanyi, wala hatutamt'ii yeyote kabisa dhidi yenu. Na mkipigwa vita lazima
tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni
waongo.
12. Pindi wakitolewa hawatatoka pamoja nao, na wakipigwa
vita hawatawasaidia. Na kama wakiwasaidia basi watageuza migongo; kisha
hawatanusuriwa.
13. Hakika nyinyi ni kitisho zaidi katika vifua vyao kuliko
Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu kitu.
14. Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipo kuwa katika vijiji
vilivyo zatitiwa kwa ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali.
Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa
wao ni watu wasio na akili.
15. Ni kama mfano wa walio kuwa kabla yao hivi karibuni.
Walionja uovu wa mambo yao. Nao watapata adhabu iliyo chungu.
16. Ni kama mfano wa Shetani anapo mwambia mtu: Kufuru. Na
akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wa walimwengu wote.
17. Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni,
wadumu humo daima; na hiyo ndiyo jaza ya madhaalimu.
18. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi
iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika
Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.
19. Wala msiwe kama wale walio msahau Mwenyezi Mungu, na
Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio wapotovu.
20. Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi. Watu wa
Peponi ndio wenye kufuzu.
21. Lau kuwa tumeiteremsha hii Qur'ani juu ya mlima, basi
bila ya shaka ungeli uona ukinyenyekea, ukipasuka kwa khofu ya Mwenyezi Mungu. Na
hiyo mifano tunawapigia watu ili wafikiri.
22. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipo kuwa
Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo onekana. Yeye ndiye Mwingi
wa rehema, Mwenye kurehemu.
23. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo
kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye
kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka,
Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo mshirikisha nayo.
24. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia
sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi
kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hikima.
|