60. SURAT AL-MUMTAH'INAH
(Imeteremka
Madina)
Sura hii imeanza kwa
kuwakataza Waumini wasiwafanye urafiki washirikina, ambao ni maadui wa Mwenyezi
Mungu na maadui zao wao, kwa kushikilia kwao ukafiri, na kumtoa Mtume wa
Mwenyezi Mungu na Waumini kwenye nyumba zao Makka. Na ikaashiria kwamba uadui
wa watu hawa kwa Waumini, ulio fichikana, hauwachi kudhihiri pale wanapo wakuta
na wakapata nguvu juu yao.
Kisha Sura ikaingia kubainisha ruwaza njema ya Ibrahim na walio kuwa pamoja
naye katika kujitenga na washirikina, na hayo waliyo kuwa wakiyaabudu badala ya
Mwenyezi Mungu, wakitangaza uadui wao kwao mpaka wamuamini Mwenyezi Mungu peke
yake. Hayo yanaonyesha kuwa huo ndio mwendo wa wanao taraji kukutana na
Mwenyezi Mungu, na wanaogopa adhabu yake.
Kisha ikabainisha makhusiano yepi yanafaa kuwa nayo na wasio kuwa Waislamu, na
yepi hayafai. Ama wale ambao hawatupigi vita katika Dini wala hawasaidii dhidi
yetu, basi ni waajibu wetu kuwafanyia wema, na kuwafanyia haki. Ama hao wanao
tupiga vita katika Dini, na wakasaidia katika kututoa kwenye nyumba zetu na
miji yetu, hao, basi, ndio Mwenyezi Mungu anatukataza kuwafanyia hisani na
kukhusiana nao.
Kisha Sura ikabainisha hukumu ya Waumini wanawake walio hamia kwenye mji wa
Kiislamu, na wakawaacha waume zao wa kishirikina; na hukumu ya wanawake wa
kishirikina ambao waume zao Waislamu wamehama, na hao wanawake wakaachwa katika
mji wa shirki.
Na ikafuatiliza kueleza kutoa ut'iifu wanawake, kwa walivyo mtolea Mtume s.a.w.
Kisha Sura ikakhitimisha, kama ilivyo anza, kwa kukataza kuwafanya urafiki
maadui walio kasirikiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuthibitisha hukumu iliyo kwisha
tolewa mwanzo wake, na ikaitilia nguvu katika kuthibitisha kwake.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Enyi mlio amini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa
marafiki mkiwapa mapenzi, na hali wao wamekwisha ikataa haki iliyo kujieni,
wakamfukuza Mtume na nyinyi kwa sababu mnamuamini Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi
wenu. Mnapotoka kwa ajili ya Jihadi katika Njia yangu na kutafuta radhi yangu,
mnafanya urafiki nao kwa siri, na Mimi nayajua mnayo yaficha na mnayo
dhihirisha. Na mwenye kufanya hayo kati yenu basi ameipotea njia ya sawa.
2. Wakikuwezeni wanakuwa maadui zenu, na wanakukunjulieni mikono
yao na ndimi zao kwa uovu. Na wanapenda muwe makafiri.
3. Hawatakufaeni jamaa zenu, wala watoto wenu Siku ya Kiyama.
Mwenyezi Mungu atapambanua baina yenu, na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo
yatenda.
4. Hakika nyinyi mna mfano mzuri kwenu kwa Ibrahim na wale
walio kuwa pamoja naye, walipo waambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi
na hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tunakukataeni; na umekwisha
dhihiri uadui na chuki baina yetu na nyinyi mpaka mtakapo muamini Mwenyezi
Mungu peke yake. Isipo kuwa kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika
nitakuombea msamaha, wala similiki chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi
Mungu. Mola wetu Mlezi! Juu yako tumetegemea, na kwako tumeelekea, na kwako
ndio marejeo.
5. Mola wetu Mlezi! Usitufanyie mtihani kwa walio kufuru.
Na tusamehe, Mola wetu Mlezi. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
6. Kwa yakini umekuwa mfano mzuri kwenu katika mwendo wao,
kwa anaye mtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kugeuka basi
hakika Mwnyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
7. Asaa Mwenyezi Mungu akatia mapenzi baina yenu na hao
maadui zenu, na Mwenyezi Mungu ni Mweza, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
8. Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu
wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi
Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.
9. Hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni kufanya urafiki na
wale walio kupigeni vita, na wakakutoeni makwenu, na wakasaidia katika
kufukuzwa kwenu. Na wanao wafanya hao marafiki basi hao ndio madhaalimu.
10. Enyi mlio amini! Wakikujilieni wanawake Waumini walio
hama, basi wafanyieni mtihani - Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua zaidi Imani
yao. Mkiwa mnawajua kuwa ni Waumini basi msiwarudishe kwa makafiri. Wanawake
hao si halali kwa hao makafiri, wala hao makafiri hawahalalikii wanawake
Waumini. Na wapeni hao wanaume mahari walio toa. Wala hapana makosa kwenu
kuwaoa mkiwapa mahari yao. Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha
ndoa zenu. Na takeni mlicho
kitoa, na wao watake walicho kitoa. Hiyo ndiyo hukumu ya Mwenyezi Mungu anayo
kuhukumuni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
11. Na
akitoroka yeyote katika wake zenu kwenda kwa makafiri, tena ikatokea mkapata
ngawira, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha mahari waliyo yatoa.
Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
12. Ewe
Nabii! Watakapo kujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba hawatamshirikisha
Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatawauwa
watoto wao, wala hawataleta uzushi wanao uzua tu wenyewe baina ya mikono yao na
miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana nao ahadi, na
uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi maghfira,
Mwenye kurehemu.
13. Enyi mlio amini! Msiwafanye rafiki zenu watu ambao
Mwenyezi Mungu amewakasirikia. Hao wamekwisha kata tamaa ya Akhera, kama
makafiri walivyo wakatia tamaa watu wa makaburini.
|