61. SURAT ASS'AF
(Imeteremka
Madina)
Sura hii imefunguka kwa
kutoa khabari kwamba viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamsabihi Mwenyezi
Mungu. Na kwamba haiwaelekei Waumini kusema wasiyo yatenda. Na hakika Mwenyezi
Mungu anapenda wawe mkono mmoja. Kisha Sura imewashutumu Wana wa Israili kuwa
ni wenye inda na ukafiri kwa kauli za Mitume wawili watukufu, nao ni Musa na
Isa s.a.w. Na kwamba wao wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuitimiza nuru yake. Na ndani ya hii Sura ipo ahadi ya Mwenyezi
Mungu - na ahadi yake ni ya kweli - kuwa ataifanya Dini hii ishinde dini zote
nyenginezo, hata walau washirikina wakichukia. Na ikakhitimishia kwa kuhimiza
Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa hali na mali, na kuwaahidi wenye
kupigana Jihadi, Mujahidina, kupata msamaha na Pepo, na mengineyo wayapendayo
Waumini, nayo ni msaada utokao kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi wa karibu. Na
wanahimizwa Waumini wawe wenye kumsaidia Mwenyezi Mungu, kama walivyo kuwa
wanafunzi wa Isa bin Mariamu. Na kwamba Mwenyezi Mungu atawaunga mkono Waumini
kwa msaada wake, na Yeye ni Mwenye kushinda katika kila kitu, Mwenye hikima ya
ukomo.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na
katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
2. Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda?
3. Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema
msiyo yatenda.
4. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana katika
Njia yake kwa safu kama jengo lilio kamatana.
5. Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa
nini mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliye
tumwa kwenu? Walipo potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke. Na
Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
6. Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili!
Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa
kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada
yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu
ni uchawi ulio dhaahiri!
7. Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anaye
mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu madhaalimu.
8. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao.
Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia.
9. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini
ya haki ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
10. Enyi mlio amini! Nikuonyesheni biashara itakayo
kuokoeni na adhabu iliyo chungu?
11. Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni
Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora
kwenu, ikiwa nyinyi mnajua.
12. Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika
Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani
za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa.
13. Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa
Mwenyezi Mungu, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!
14. Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu,
kama alivyo sema Isa bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu
kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu!
Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi
tukawaunga mkono walio amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.
|