66. SURAT ATTAH'RIIM
(Imeteremka
Madina)
Sura hii inaashiria jambo
ambalo lilimuudhi Nabii s.a.w. katika baadhi ya wake zake; akajizuilia na
baadhi ya mambo ambayo nafsi huyapenda na Mwenyezi Mungu amehalalisha. Na
inawahadharisha wake zake na matokeo ya waliyo yatenda. Kisha Sura ikaingia
kuwaamrisha Waumini wajikinge nafsi zao na ahali zao na Moto ambao kuni zake ni
watu na mawe. Na ikabainisha kwamba haukubalii udhuru wa makafiri Siku ya
Kiyama. Na inawataka Waumini watubu kweli kweli, na Mtume s.a.w. ende kupambana
kwa Jihadi na makafiri na wanaafiki, na awe mgumu kwao. Na inakhitimisha kwa
kupiga mifano kwamba wema wa waume hautazuia adhabu isiwafikie wake zao wakiwa
wao wamepotoka, na kwamba uharibifu wa waume hauwadhuru wake zao ikiwa hao wake
wamesimama sawa sawa. Kwani kila nafsi ina dhamana kwa vitendo vyake mwenyewe.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Ewe
Nabii! Kwa nini unaharimisha alicho kuhalilishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta
kuwaridhi wake zako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
2. Hakika
Mwenyezi Mungu kakupeni Sharia ya kufungua viapo vyenu, na Mwenyezi Mungu ni
Mola wenu. Na Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
3. Na
Nabii alipo mwambia mmoja wa wake zake jambo la siri. Basi alipo litangaza yule
mke, na Mwenyezi Mungu akamdhihirishia Mtume, alimjuvya sehemu na akaacha
sehemu nyengine. Alipo mwambia hayo, huyo mke akasema: Nani aliye kwambia haya?
Mtume akasema: Kaniambia Mjuzi Mwenye khabari zote!
4. Kama
nyinyi wawili hamkutubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwisha elekea
huko. Na mkisaidiana dhidi yake (Mtume), basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye
kipenzi chake, na Jibrili, na Waumini wema, na zaidi ya hayo Malaika pia
watasaidia.
5. Asaa
Mola wake Mlezi, akikupeni talaka, akampa wake wengine badala yenu nyinyi,
walio bora kuliko nyinyi, wanynyekevu, Waumini, wat'awa, walio tubu, wenye
kushika ibada, wafanyao kheri, wajane na wanawari.
6. Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na
Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu,
hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa.
7. Enyi mlio kufuru! Msilete udhuru leo. Hakika mnalipwa
mliyo kuwa mkiyatenda.
8. Enyi mlio amini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya
kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika
Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii
na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia,
na huku wanasema: Mola wetu Mlezi! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie!
Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
9. Ewe
Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na kuwa mgumu kwao! Na makaazi yao ni Jahannamu.
Na hayo ni marejeo mabaya.
10.
Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walio kufuru: mke wa Nuhu na mke wa Lut'i.
Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu. Lakini
wakawakhuni waume zao, nao wasiwafae kitu. Na ikasemwa: Ingieni Motoni
pamoja na wanao ingia!
11. Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walio amini - mkewe
Firauni, alipo sema: Mola wangu Mlezi! Nijengee kwako nyumba Peponi, na uniokoe
na Firauni na vitendo vyake, na uniokoe na watu madhaalimu.
12. Na Mariamu binti wa Imrani, aliye linda ubikira wake,
na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi
na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa wat'iifu.
|