67. SURAT AL-MULK
(Imeteremka
Makka)
Sura
hii inaitwa Surat Al-Mulk kwa kutokana na neno Al-Mulk, yaani Ufalme, linalo
tokea katika Aya ya kwanza katika Sura. Na muhimu ya makusudio ya Sura hii
tukufu ni kuelekeza fikra na nadhari zizingatie athari ya uweza wa Mwenyezi
Mungu ulio zagaa katika nafsi za watu na katika viumbe vya Mwenyezi Mungu
mnavyo viona katika ardhi na mbinguni upeo wa macho yenu, ili hayo yawe ndiyo
njia ya kupelekea kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na pia Sura hii
inabainisha hali ya makafiri ambao watatupwa katika Jahannamu, na
watasikilizana mikoromo yao, na wataungua katika Moto wake, na wataungama madhambi
yao, na watajuta kwa watavyo ishia, watapo wauliza Malaika kwa kuto mwitikia
Mtume alipo waita na akawahadharisha.
Na ama walio mkhofu Mola wao Mlezi, na wakamuamini, hao watapata maghfira na
msamaha kwa makosa yaliyo waporonyoka, na ujira mkubwa kwa mema waliyo
yatanguliza na wakayatenda.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye
ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
2. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani
miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye
msamaha.
3. Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti
yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote?
4. Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea
mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka.
5. Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na
tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa
nguvu.
6. Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya
Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo!
7. Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku
inafoka.
8. Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa
kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji?
9. Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini
tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi
hamumo ila katika upotovu mkubwa!
10. Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na
akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni!
11. Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa
Motoni!
12. Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu,
watapata maghfira na ujira mkubwa.
13. Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni
Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
14. Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye
khabari?
15. Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi
tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio
kufufuliwa.
16. Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa
hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika!
17. Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye
hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu?
18. Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla
yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu?
19. Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo
zikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika
Yeye ni Mwenye kuona kila kitu.
20. Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya
Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu.
21. Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye
akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki.
22. Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu
zaidi, au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka?
23. Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na
akakupeni masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu.
24. Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na
kwake mtakusanywa.
25. Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli?
26. Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na
hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha.
27. Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru
zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba.
28. Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi
na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na
adhabu chungu?
29. Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na
juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri.
30. Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini,
nani atakueleteeni maji yanayo miminika?
|