69. SURAT AL-H'AAQQAH
(Imeteremka
Makka)
Sura hii tukufu
inaeleza hali za Kiyama, na imetaja yaliyo wasibu watu wa mataifa yaliyo tangulia,
ya kuteketezwa, na kuchukuliwa kwa nguvu na shida walipo kadhibisha. Na imetaja
namna litavyo pulizwa baragumu, na mageuzi na kuondoka yatakayo zisibu ardhi na
milima na mbingu. Na yatakayo tokea baada ya hayo ya kuletwa watu kwa ajili ya
hisabu, na kubashiriwa watu wa mkono wa kulia kwa malipo ya ukarimu na neema za
daima watakazo zipata, na maonyo ya watu wa kushoto na adhabu chungu. Tena Sura
ikakhitimisha kwa kutaja ukweli wa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. katika Ujumbe
alio ufikisha, na ukweli wa Qur'ani ambao ndio ni Haki iliyo yakini.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Tukio la haki.
2. Nini hilo Tukio la haki?
3. Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki?
4. Thamudi na A'di waliukadhibisha Msiba unao situsha.
5. Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno.
6. Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika.
7. Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila
ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi
ndani.
8. Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki?
9. Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa
chini juu, walileta khatia.
10. Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola
akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu.
11. Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina,
12. Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio
linalo sikia liyahifadhi.
13. Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu,
14. Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo
mmoja,
15. Siku hiyo ndio Tukio litatukia.
16. Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu
kabisa.
17. Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu
ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi.
18. Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote
yenu.
19. Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa
kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!
20. Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu.
21. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza,
22. Katika Bustani ya juu,
23. Matunda yake yakaribu.
24. Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya
mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita.
25. Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa
kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu!
26. Wala nisingeli jua nini hisabu yangu.
27. Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa.
28. Mali yangu hayakunifaa kitu.
29. Madaraka yangu yamenipotea.
30.
(Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu!
31. Kisha mtupeni Motoni!
32. Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa
sabiini!
33. Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu
Mtukufu,
34. Wala hahimizi kulisha masikini.
35. Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu,
36. Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni.
37. Chakula hicho hawakili ila wakosefu.
38. Basi naapa kwa mnavyo viona,
39. Na msivyo viona,
40. Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye
hishima.
41. Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana
mnayo yaamini.
42. Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka.
43. Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
44. Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu,
45. Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia,
46. Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo!
47. Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza
kutuzuia.
48. Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu.
49. Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni
mwenu wapo wanao kadhibisha.
50. Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao
kataa.
|