72. SURAT AL-JINN
(Imeteremka
Makka)
Mwenyezi Mungu Mtukufu
amemuamrisha Mtume wake s.a.w. katika Sura hii tukufu awafikishie watu aliyo
funuliwa yeye kwa wahyi, kwamba majini wameisikiliza Qur'ani na wameitikia wito
wake, na kuwapa khabari kwa yaliyo wapata wapumbavu wao na wema wao, na yaliyo
kuwa kutokana na kukaa kwao kusikiliza kwa wizi, na kufukuzwa kwao hivi sasa.
Na Aya za Sura hii zinaeleza khabari za hao wanao nyatia kwenye njia ya Uislamu
na kuupinga, na ikasimulia juu ya kuisafishia misikiti kwa ajili ya kumuabudu
Mwenyezi Mungu tu peke yake, na juu ya wito wa Mtume kumwendea Mwenyezi Mungu,
na majini kumzunguka Mtume, na ikaeleza kwa kuwekea mipaka lipi aliwezalo Mtume
na lipi ambalo haliwezi, na ikahadhirisha wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume
watahadhari na Jahannamu na kubakia humo milele.
Na mwishoe Sura ikakhitimisha kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye
khusika na kuijua ilimu ya ghaibu, mambo yasiyo onekana, na humdokezea anaye
mteuwa katika viumbe ili awe ni Mtume wa kuuhifadhi Wahyi kwa kuulinda mpaka
awafikishie watu kwa utimilivu. Na Mwenyezi Mungu anayajua hayo.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini
lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu!
2. Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala
hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi.
3. Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka
kabisa; hana mke wala mwana.
4. Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema
uwongo ulio pindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu.
5. Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo
Mwenyezi Mungu.
6. Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa
wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi.
7. Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi,
ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume.
8. Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi
wenye nguvu na vimondo.
9. Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao
ili kusikiliza; lakini sasa anaye taka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia!
10. Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanao kaa
kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu.
11. Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu
ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.
12. Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani,
wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia.
13. Nasi tulipo usikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye
kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa.
14. Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu
wanao acha haki. Basi walio silimu, hao ndio walio tafuta uwongofu.
15. Na ama wanao acha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu.
16. Na lau kama wangeli simama sawasawa juu ya njia tungeli
wanywesha maji kwa wingi,
17. Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anaye puuza kumkumbuka Mola
wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu.
18. Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi
msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.
19. Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu alipo simama kumwomba,
wao walikuwa karibu kumzonga!
20. Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala
simshirikishi Yeye na yeyote.
21. Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala
kukuongozeni.
22. Sema: Hakika hapana yeyote awezae kunilinda na Mwenyezi
Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipo kuwa kwake Yeye tu.
23. Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na
risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata
Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.
24. Hata watakapo yaona wanayo ahidiwa, ndipo watakapo jua
ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.
25. Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayo ahidiwa, au
Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu.
26. Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii
yeyote siri yake,
27. Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea
walinzi mbele yake na nyuma yake.
28. Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao
Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote walio nayo, na amedhibiti idadi ya kila
kitu.
|