82. SURAT AL-INFIT'AAR
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeeleza baadhi ya
vitisho vya Saa ya Kiyama kwa njia ya kutangaza kuwa hakika litatokea jambo katika
siku ambayo kila mtu atajua nini alilo litanguliza na nini alilo liakhirisha.
Tena Aya zikaingia kumhadharisha mwanaadamu aliye danganyika na Mola wake Mlezi
aliye muumba akamweka sawa, akamjenga kwa namna ya pekee, na kwa umbo bora
kabisa. Inathibitisha Sura kuwa huyo mtu anaikadhibisha Siku ya Malipo, na
inatilia mkazo kuwepo Malaika juu yake, walinzi mahashumu, waandishi. Na
ikamalizia kusema kuwa watu wema watapata neema. Na wapotovu hawatapata ila
Jahannamu, watakayo iingia Siku ya Kiyama, siku ambayo nafsi haitoweza
kuimilikia nafsi nyengine chochote. Na amri yote itakuwa ni ya Mwenyezi Mungu
tu.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Mbingu itapo chanika,
2. Na nyota zitapo tawanyika,
3. Na bahari zitakapo pasuliwa,
4. Na makaburi yatapo fukuliwa,
5. Hapo kila nafsi itajua ilicho tanguliza, na ilicho
bakisha nyuma.
6. Ewe
mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu?
7. Aliye
kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha,
8. Katika
sura yoyote aliyo ipenda akakujenga.
9. Sivyo
hivyo! Bali nyinyi mnaikanusha Siku ya Malipo.
10. Na
hakika bila ya shaka wapo walinzi juu yenu,
11.
Waandishi wenye hishima,
12.
Wanayajua mnayo yatenda.
13. Hakika
wema bila ya shaka watakuwa katika neema,
14. Na hakika
waovu bila ya shaka watakuwa Motoni;
15.
Wataingia humo Siku ya Malipo.
16. Na
hawatoacha kuwamo humo.
17. Na
nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
18. Tena
nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
19. Siku
ambayo nafsi haitakuwa na madaraka yoyote juu ya nafsi; na amri yote siku hiyo
ni ya Mwenyezi Mungu tu.
|